DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kuwa ifikapo Januari 2025, wafanyabiashara wote wa jijini Dar es Salaam wataanza rasmi kufanya biashara saa 24.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema mpango huo unalenga kuimarisha uchumi wa mkoa, kuongeza mapato ya serikali na kutoa fursa za ajira.
Ameeleza kuwa maandalizi ya ufungaji wa kamera za CCTV na taa za barabarani yanaendelea ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unadumishwa.
“Tunahakikisha mkoa wetu wa Dar es Salaam unakuwa na mazingira bora ya kufanya biashara muda wote, na tayari tunashirikiana na viongozi wa halmashauri kuimarisha maeneo yanayofaa kwa biashara za masaa 24,” amesema Chalamila.
Aidha ameongeza kuwa mpango huo utaimarisha uchumi na kuwanufaisha wafanyabiashara na wakazi wa jiji hilo.
“Serikali inatarajia kutoa mwongozo mzuri wa ufanyaji biashara na utekelezaji wa mpango huo kabla ya kuanza rasmi Januari 2025,”amesema.