Biashara Malawi, Afrika Kusini ilinde rasilimali, uhusiano

WIKI iliyopita niliandika makala yenye kichwa cha habari: ‘Wafanyabiashara Tanzania wasiwe ‘yatima’ Afrika Kusini na Malawi’.
Makala hayo yalisisitiza kuwa, wafanyabiashara wa Tanzania si yatima na katu wasifanywe yatima wa kibiashara wanapopeleka mazao ya biashara katika nchi hizo jirani na marafiki wa Tanzania yaani Malawi na Afrika Kusini.
Makala hayo yalitokana na Watanzania kupata taarifa zisizofurahisha kuhusu uhusiano wa kibiashara unaovurugwa na Afrika Kusini na Malawi dhidi ya Tanzania.
Kwamba Aprili 17, mwaka huu Serikali ya Malawi ilitoa tamko kuzuia baadhi ya mazao ya Watanzania kuingia nchini humo. Mazao hayo ni pamoja na ndizi, mchele, tangawizi na mahindi. Mbali na Malawi, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe pia akaeleza juhudi za miaka mitano za Serikali Tanzania kutaka kufunguliwa kwa soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio.
Akasema, “Inatukumbusha jinsi pia, tulivyohangaika kwa miaka 10 kufungua soko la zao la parachichi mpaka pale tulipoamua kutaka kuzuia mazao yao kuingia kwetu. Tunaona mwelekeo ni uleule.”

Huku ikiwa imeshangazwa na uamuzi huo wa majirani na rafiki hao wa Tanzania kibiashara, kupitia kwa Waziri Bashe Serikali ya Tanzania nayo sasa ikafikia hatua ya kuweka msimamo kuwa, inawasiliana kwa mara ya mwisho na serikali za Afrika Kusini na Malawi ili ziruhusu mazao ya Tanzania kuingia katika nchi hizo vinginevyo, ‘basi’ maana ‘utamu wa biashara ni kutoa na kupokea’.
Si siri, Serikali ya Tanzania ilifikia uamuzi huo wa kutoa makataa (muda wa mwisho) kwa nchi hizo kwani wafanyabiashara wa Tanzania walikuwa wanateseka katika nchi ambazo ni jirani na rafiki zao kibiashara bila sababu za msingi huku kila kukicha hasara itokanayo na bidhaa zao kukwama ikiongezeka.
Waziri Bashe kwa niaba ya Serikali ya Tanzania akasimama na kutoa msimamo thabiti kuwa, endapo nchi hizo zitakuwa hazijaruhusu mazao ya wafanyabiashara wa Tanzania kuingia ifikapo Jumatano (Aprili 23, 2025), Wizara ya Kilimo itazuia mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi zisiingie Tanzania.
Anasema, “Aidha, hatutaruhusu zao lolote kutoka nchi hizi mbili kupita ndani ya nchi yetu iwe kwenda Bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote kama tulivyofanya mwaka jana hadi wakatufungulia.” Anaongeza: “Na pia kwa kuwa tumekuwa tukiwauzia mbolea, tutazuia mbolea kwenda Malawi.”
Bashe anasema utekelezwaji wa notisi unaanza Aprili 23, 2025 kama serikali itakuwa haijapata mrejesho kutoka Malawi na Afrika Kusini. Akaweka ukweli na uwazi kwa Watanzania kupitia ukurasa wake wa ‘X’ alipoandika: “Ifahamike kwamba kama, waziri mwenye dhamana nimefanya jitihada zote za kuwasiliana na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila kupata majibu yoyote.”
Katika makala hayo ya Aprili 22, 2025, mwandishi anaandika, “Kwa mtazamo wangu, msimamo wa Bashe unapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote wakiwamo hasa wafanyabiashara ambao ndio hasa walengwa na waathirika wakubwa wa hilo linalotokea Malawi na Afrika Kusini na ndio wanaoteseka.”
Yakaongeza: “Afrika Kusini na Malawi wasitake kuwanyanyapaa wafanyabaishara wa Tanzania kama vile wanataka kuwaona ni ‘yatima masikini. Lazima Watanzania wajiulize; ‘Kama sisi ni maskini, mbona wanakuja kwetu.” Wataalamu wa mambo ya uchumi wanasema uchumi wa nchi hukua inapouza zaidi nje ya nchi kuliko inaponunua kutoka nje ya nchi.
Kwa msingi huo, nchi inapotaka iuze kwako bila wewe kuiuzia maana yake inakutakia mabaya yaani, ‘wewe ukonde, yeye anenepe’ kiuchumi. Hilo halikubaliki. Baadhi ya watu walipiga simu kuunga mkono wa serikali kama yaliyosema makala, lakini isivyo bahati ni kwamba, ‘sikio la kufa halisikii dawa’ na ng’ombe hajui umuhimu wa mkia wake hadi unapokatika.’
Hata baada ya Tanzania kutoa onyo kwa nchi hizo kuwa endapo hazitarekebisha uamuzi kwa kuondoa zuio hilo ndani ya siku saba, Tanzania nayo itazuia uingizaji wa bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini, ziliendelea kukaa kimya.
Ikawa hivyo, nchi hizo zikidhani Tanzania inatishia kwa ‘maji ya moto yasiyounguza nyumba’ zikapuuza na kuendelea kukaa kimya bila marekebisho yoyote kuondoa zuio.
Ndipo sasa thamani ya mkia wa ng’ombe ikaonekana baada ya Jumatano hiyo ya Aprili 23, mwaka huu Tanzania nayo kupitia Wizara ya Kilimo, ikatangaza marufuku mazao ya kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini na kusitisha usafirishaji wa bidhaa hizo kupitia Tanzania kuelekea Malawi ikiwamo mbolea iliyokuwa itumike kwa ajili ya kilimo katika msimu ujao nchini Malawi.

Kinachofurahisha ni kwamba, Jumamosi (Aprili 26, 2025), Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe imetangaza kuondoa zuio hilo la biashara na usafirishaji wa mazao ya kilimo kati ya Tanzania na nchi za
Malawi na Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa Bashe, Tanzania imeamua kuondoa vizuizi vyote ili kutoa nafasi kwa mchakato wa kidiplomasia kuendelea kutokana na kuwapo sasa kwa mawasiliano rasmi kutoka nchi hizo na nia yao ya kutaka majadiliano ya pamoja.
Bashe amenukuliwa akisema, “Wizara ya Kilimo inaondoa mazuio yote yaliyowekwa kwa nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia Aprili 26, 2025 tukiamini kuwa majadiliano yanayoendelea yatatoa suluhisho la kudumu.”
Kwamba, Serikali ya Malawi imethibitisha kutuma ujumbe rasmi utakaowakilishwa na Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo kwa ajili ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania jijini Dodoma Mei 2, mwaka huu (Ijumaa hii).
Kuhusu Afrika Kusini, waziri huyo anasema majadiliano kati ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo ya
Tanzania kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu na mamlaka husika za Afrika Kusini yanaendelea
ili kuhakikisha masuala ya afya ya mimea na masoko kwa maslahi ya nchi zote mbili yaani Tanzania na Afrika Kusini yanatakiwi yaani ‘tupate wote’ na si ‘mimi nikuwezeshe kupata, wewe uniwezeshe kukosa.’
Kimsingi kinachowafurahisha Watanzania na kuahidi kuendelea kuiunga mkono serikali yao hususani katika sakata hili, ni msimamo chanya usioyumba wa serikali kupitia kwa Waziri Bashe anayesema Tanzania itaendelea
kulinda maslahi ya taifa kwa kuhakikisha biashara huru yenye tija kwa mazao ya kilimo inafanyika kwa kuzingatia kanuni za afya ya mimea, rasilimali za nchi na uhusiano wa kidiplomasia.
Ndio maana Watanzania wengi wanasema biashara baina ya Tanzania, Malawi na Afrika Kusini ilinde
rasilimali na uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia ili pande zote zinufaike kwa rasilimali zilizopo upande
mmoja kufukia mashimo ya upande mmoja na si faida ya upande mmoja maana wafanyabiashara wa
Tanzania si yatima na nchi yao imebarikiwa kuwa na rasilimali lukuki ambazo pia hazipo katika nchi nyingine.