Biashara ya kaboni kufungua ajira vijijini

UTURUKI; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amesema biashara ya kaboni ina uwezo wa kufungua fursa za ajira na kuongeza kipato kwa wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini, kupitia shughuli za upandaji na utunzaji wa miti.

Masauni amesema biashara hiyo inatoa fursa kwa wananchi kushiriki katika soko la kaboni na kunufaika kiuchumi, huku wakichangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 12, 2026, jijini Antalya, Uturuki, ambako anashiriki Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), amesema mnyororo mzima wa biashara hiyo unaweza kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa wananchi.

Ameeleza kuwa fursa hizo zinapatikana katika hatua mbalimbali, kuanzia uandaaji wa miche, upandaji na utunzaji wa miti hadi ushiriki katika soko la kaboni.

Amesema amekuwa akielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika biashara hiyo na namna ya kuzitumia kujinufaisha kiuchumi.

Masauni amesisitiza kuwa biashara ya kaboni ina nafasi mbili muhimu katika maendeleo ya nchi, ambazo ni kuchochea uhifadhi wa mazingira na kuongeza kipato kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli zinazohusiana na upandaji na utunzaji wa miti.

Aidha, amesema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za kuimarisha biashara hiyo nchini, ikiwemo kuanzisha Kituo cha Kitaifa cha Kusimamia Biashara ya Kaboni na kufanya maboresho ya sera na sheria ili kuweka mazingira bora ya utekelezaji wake.

Amesema hatua hizo zinalenga kuweka mazingira yatakayowawezesha wananchi kushiriki katika biashara hiyo na kunufaika na fursa zake, huku Tanzania ikiendelea kuimarisha juhudi za uhifadhi endelevu wa mazingira.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button