Bibi atuhumiwa kuua mjukuu kisa salamu
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamtafuta Christina Kishiwa anayetuhumiwa kumuua mjukuu wake, Sophia Nduni (4).
Kamanda Polisi wa mkoa huo, Janeth Magomi amesema mtoto huyo ameaga dunia baada ya kupigwa na kitu chenye ubapa kichwani.
Inadaiwa bibi wa mtoto huyo alimpiga baada ya kutokumsalimia alipoamka asubuhi ya Septemba 29 katika Mtaa wa Nyakato, Kata ya Nyasubi, Manispaa ya Kahama.
SOMA: Watu 18 wanaswa kwa makosa mbalimbali Shinyanga
Kamanda Magomi amesema mtoto huyo alikuwa akiishi na mama yake mzazi na bibi yake na siku ya tukio alipoamka asubuhi bibi yake alimtaka amsalimie, mtoto huyo akakaa kimya.
Amesema baada ya tukio hilo Christina alitoroka, hivyo polisi wanaendelea kumtafuta.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato, Kata ya Nyasubi, Hussein Mwita amesema uongozi wa mtaa haukupata taarifa kwa wakati kuhusu tukio hilo.
“Ni kweli tukio limetokea mtaani kwangu na mwenye nyumba ametokomea kusikojulikana na wakati naingia madarakani nilikuta kuna kumbukumbu za mtuhumiwa kumchoma msichana wake wa kazi moto mikononi, hivyo sio tukio lake la kwanza kufanya ukatili,” amesema Mwita.
Amesema kabla ya mtuhumiwa kubainika, aliandaa mazingira ya kwenda kumzika marehemu kijijini kwao lakini watu walibaini na kutoa taarifa kwenye uongozi wa mtaa na jeshi la polisi na kuanza kumtafuta.
Inadaiwa mara kwa mara Christina alikuwa akimpiga mtoto huyo na katika tukio la Septemba 29 alitumia bomba la plastiki na kisha alimbamiza ukutani.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dk Marco Mushi amesema Septemba 29, mwaka huu saa tatu usiku walipokea mwili wa mtoto huyo akiwa amekufa.
Dk Mushi amersema baada ya kuufanyia uchunguzi wa awali, walibaini mtoto huyo alipigwa kichwani na kitu chenye ubapa na pia alibainika mwili ulikuwa na majeraha maeneo ya kichwani, kifuani, tumboni na mikononi.



