JESHI la Polisi mkoani Shinyanga limefanikiwa kukamata watu 81 kwa kuhutumiwa makosa mbalimbali katika kipindi cha kuanzia mwezi Novemba hadi Desemba mwaka huu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Janeth Magomi amesema hayo leo mbele ya waandishi wa habari nakueleza kuanza oparesheni hiyo iliyokuwa na lengo la kubaini na kuzuia uhalifu .
Kamanda Magomi amesema watu hao licha ya kukamatwa kwa kutuhumiwa kwa makosa wapo waliokutwa na madini ya dhahabu bandia gramu 250, bangi gramu 9000, mirungi bunda tisa pamoja na pombe ya Moshi lita 113.
Kamanda Magomi amesema polisi waliokuwa doria walifanikiwa kukamata silaha aina ya Gobore katika kijiji cha Bugomba A kata ya Ulewe Halmashauri ya Ushetu.
“Gobore hilo lilikuwa limepakizwa kwenye baiskeli na mtu ambaye alikuwa akiendesha alitelekeza nakufanikiwa kukimbia lakini wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa,” amesema Magomi.
Kamanda Magomi alisema kesi 18 zimepata mafanikio ambapo watuhumiwa wanne wamefungwa maisha huku kesi moja ya ubakaji mshtakiwa alihukumiwa miaka 30 kwenda jela.
Kamanda Magomi amesema wamefanikiwa kukamata makosa 5,376 ya usalama barabarani ikiwa makosa ya kwenye magari ni 3,767 na makosa ya bajaji na pikipiki ni 1,609.
“Tumefanya mikutano 97 ya utoaji elimu juu ya kuzuia uhalifu na kuondoa ukatili kupitia vyombo vya habari tukiwataka wananchi kushirikiana na jeshi hili,” amesema Magomi