WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 19 wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 utakaonufaisha kaya 5,940 mkoani Tabora.
Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Robert Dulle amesema hayo leo Novemba 07 mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Chacha wakati wa kumtambulisha mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo.
SOMA: Kapinga aiagiza REA kufikisha umeme vitongojini
“Napenda kuwafahamisha wananchi wa Tabora kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan ameridhia kiasi cha shilingi 19,057,015,682.55 kitumike kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 mkoani hapa na leo hii tupo hapa kumtambulisha mkandarasi anayetekeleza mradi huu,”amesema Dulle.
Mhandisi Dulle amesema mradi unatekelezwa ndani ya majimbo yote 12 ya mkoani humo kwa muda wa miaka miwili na utakamilika Agosti, 2026 ambapo kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amemuelekeza Mkandarasi kuhakikisha anakamalisha kazi hiyo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa huku akiipongeza REA kwa kuendelea kutimiza dhamira ya Rais Dk. Samia kwa vitendo.
Naye Meneja wa Mradi kutoka Kampuni ya Sinotec Company Ltd ya China, Mhandisi Alphred Kessy alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa mradi kukamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.