ZAIDI ya Sh bilioni 20 zitatumika kusambaza umeme kwenye vitongoji 105 katika majimbo ya Mkoa Iringa kupitia mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji awamu ya pili (HEP II) unaotekelezwa kwa miaka miwili kati ya sasa na Septemba 2026.
Kupelekwa umeme katika vitongoji hivyo kutafanya jumla ya vitongoji vyenye umeme kufikia 1,293 kati ya vitongoji 1,853 vya mkoa huo.
Msimamizi wa miradi ya REA wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Dunstan Kalugira amesema utakapokamilika mradi huo utaziunganisha kaya za vitongoji hivyo na umeme, na unatazamiwa kuboresha maisha ya watu kwa kuongeza upatikanaji wa nishati, kuboresha huduma za afya, elimu, na fursa za kiuchumi.
Akiutambulisha mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa, Peter Serukamba amesema mradi huo utasaidia kupunguza pengo la upatikanaji wa umeme kati ya maeneo ya mijini na vijijini, hatua ambayo itachangia katika kuongeza kasi ya maendeleo.
“Tunaamini kwamba kwa kupeleka umeme hadi ngazi ya vitongoji, tutawezesha wananchi wengi zaidi kujihusisha na shughuli za kiuchumi, kupata elimu bora na huduma bora za afya,” amesema.
SOMA: Dk Biteko aipongeza REA umeme vijiji vya Iringa
Akiupokea mradi huo, Mkuu wa Mkoa alisema wamepokea taarifa hizi kwa furaha, wakitarajia kwamba upatikanaji wa umeme utachangia kuboresha hali za maisha ya watanzania wote.
“Watu wetu watakuwa na uwezo wa kuanzisha biashara ndogo ndogo, watoto wetu watasoma vizuri, na hata huduma mbalimbali zikiwemo za afya na elimu zitaboreshwa,” amesema Serukamba.
Alisema mradi huo unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya viwanda vidogo vidogo, sekta ya kilimo, na kuongeza uzalishaji katika sekta ya usindikaji wa mazao.
“Kwa kuzingatia kwamba nishati ni kiungo muhimu kwa maendeleo, utekelezaji wake utafungua milango kwa fursa nyingi zaidi za kiuchumi kwa wananchi wa kawaida,” alisema na kuongeza kuwa mkoa wake una jumla ya vijiji 360 vyote vikiwa na huduma ya umeme.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kampuni ya STEG International Services inayotekeleza mradi huo, Aymen Louhaichi alisema watajitahidi kuutekeleza mradi huo ndani ya wakati ili kufikia matarajio ya nchi na watu wake.