Bil 21/- kutumika elimu ya Sekondari njia mbadala

SERIKALI imeiwezeshaTaasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Sh bilioni 21.8 kwa kipindi cha miaka minne ili kutekeleza kazi mbalimbali za kuimarisha ubora wa elimu kupitia Mradi wa Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP) kuanzia mwaka 2021/ 2022 hadi 2024/2025.
Mkuu wa Taasisi hiyo ,Profesa Michael Ng’umbi amesema hayo mjini Morogoro alipomkaribisha Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la Taasisi hiyo, Profesa Zacharia Mganilwa kufungua mafunzo ya matumizi ya “ Force Account “ kwa watekelezaji wa ujenzi na ukarabati majengo ya Taasisi hiyo nchini.
Profesa Ng’umbi amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali Kuu kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ili kutekeleza mradi huo wa miaka mitano ulioanza mwaka 2020/2021 na kifikia ukomo mwaka 2025/2026.
“ Taasisi yetu ina jukumu la kuimarisha utolewaji wa program hii na kwa sasa ipo katika mwaka wa mwisho wa utekelezaji” amesema .

Profesa Ng’umbi amesema lengo la mradi ni kuongeza ufikiwaji wa wasichana walioshindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa, waliacha shule kutokana na mazingira magumu, kupata ujauzito au ndoa za utotoni.
“ Mradi huu umewalenga wasichana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 21 na malengo makuu ni kuwafikia wasichana wapatao 12,000 nchini kote hadi kipindi cha mradi kumalizika’’anasema .
Amesema mradi huo umelenga kuwapatia wasichana na wavulana mazingira bora ya kujifunza,kuongeza ufaulu kwa wahitimu wa elimu ya sekondari kwa njia mbadala kwa kiwango cha kuanzia daraja la kwanza hadi ya tatu.
Mbali na hayo Profesa Ng’umbi amesema mradi huo pia umewezesha kazi za ukarabati wa majengo mbalimbali ya Taasisi katika kampasi zake,vituo vilivyopo kila mkoa nchini, madarasa, vyoo na hosteli.
Amesema katika kipindi kilichobaki mradi umelenga kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya majengo ya matumizi mbalimbali wakiwemo madarasa.

Profesa Ng’umbi amesema ujenzi majengo hayo inafanyika katika mikoa ya Lindi, Kagera ,Arusha , Katavi , Mbeya ,Mara na Iringa ambapo utafanyika ujenzi wa Hosteli yenye uwezo wa wanafunzi 80.
Mkuu wa taasisi hiyo amesema hadi mwaka 2024 mradi umewezesha kuwarejesha shuleni wasichana wapatao 10,239 waliokatiza masomo ya Sekondari kabla ya kufikia ukomo wake wa miaka mitano.


