DAR ES SALAAM; MAHAKAMA Kuu Kituo cha Usuluhishi kimefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni tano kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, baada ya kusuluhisha kesi 42 kati ya mashauri 140.
Akitoa taarifa hiyo jana Dar es Salaam, Naibu Msajili Augustina Mmbando alisema mahakama hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Juni 30, mwaka huu wamepokea mashauri 152 na kati ya hayo yaliyofaulu kwenye usuluhishi ni 42 huku mashauri 98 yakiendelea kusikilizwa.
Mmbando alisema usuluhishi umesaidia kuokoa Sh bilioni tano na kwamba wanatarajia kuokoa zaidi ya Sh bilioni 10 kwa sababu endapo mashauri hayo yangeenda kusikilizwa katika mahakama za kawaida, yangechukua muda mrefu na gharama za uendeshaji wa kesi zingeongezeka.
“Fedha hizi zinaokolewa kwa namna hii, kama kuna mtu anakudai shilingi milioni 500 mnapokuja kusuluhisha mdaiwa anaweza kukuomba akulipe milioni 200 na ukikubali basi fedha iliyobaki inakuwa faida kwa sababu mngeenda katika mahakama za kawaida ni lazima ungelipa fedha yote,” alifafanua.
Alitaja faida za usuluhishi kuwa ni pamoja na kuokoa gharama na muda wa wadai kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo tofauti na kwenda mahakamani, pia hurudisha mahusiano yaliyopotea kati ya pande hizo.
“Utaratibu tunaoutumia tunawaeleza wateja wetu kutokuja na misimamo yao hasi kuhusu mashauri wanayoleta, kabla shauri halijaanza tunawapa elimu ya faida za usuluhishi. Sisi hatutumii vifungu vya sheria katika kusuluhisha bali tunatumia njia ya mazungumzo kwa kumsikiliza mmoja mmoja,” alisisitiza.
Mashauri mengi yanayopelekwa katika kituo hicho yanahusu migogoro ya ardhi kutoka Mahakama Kuu, divisheni ya Ardhi na mengine ya kuvunja mikataba na kwamba hawahusiki na mashauri ya ndoa.
“Mashauri yanayoletwa kwetu ni yale ya madai yanayoanza sio yanayotokana na rufaa, maombi au mapitio. Kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya madai mashauri yakifika eneo fulani, lazima lipite kwenye usuluhishi na endapo majaji au mahakimu watayasikiliza bila kuzingatia kipengele hiki na hata kama ametoa hukumu, itahesabika hakuna mshindi na litaanza upya,” aliongeza.
Akielezea namna wanavyotoa elimu, Mmbando alisema kila siku ya Jumanne ya kwanza ya mwezi na mwisho wa mwezi kuanzia saa 2:00 hadi 3:00 asubuhi, wanatoa elimu ya usuluhishi kwa wateja wanaosubiri kusikiliza kesi mbalimbali Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya Ardhi ni siku ya Jumatano.
Mmbando alieleza utaratibu huo umewawezesha kuwafikia wateja zaidi ya 657 wa ana kwa ana na kwa kipindi cha Januari hadi Juni hivyo, matarajio yao kuwafikia wateja 1,000.
Kwa mujibu Mmbando awali masuala ya usuluhishi hayakuwa na miongozo lakini tangu Machi 14, mwaka huu Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma alitoa muongozo ambao umetoa utaratibu namna ya kufanya shughuli hizo za usuluhishi.