Taasisi yamsaidia mabati, saruji mwenye ulemavu

DAR ES SALAAM; Taasisi ya Tanzania Generation Care imetoa msaada wa mifuko ya saruji, bati pamoja na matofali kwa ajili ya kumsaidia mlemavu wa macho, Paulo Lupita, mkazi wa Tabata Mawenzi, Dar es Salaam, ambaye nyumba yake imebomoka na hivyo kulazimika kulala nje.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa taasisi ya Tanzania Generation Care, Fauzia Mbwana, amesema taasisi hiyo imeguswa kumsaidia kutokana na hali yake ya uhitaji.

Amesema Lupita pamoja na mke wake ni watu wenye ulemavu na wanahitaji msaada ili kuboresha maisha yao, hasa baada ya kulazimika kuishi nje kufuatia kubomoka kwa nyumba yao.

Mbwana amesema wanaamini msaada huo utasaidia kutatua changamoto inayowakabili kwa kuwezesha ujenzi wa sehemu ya nyumba ambayo ukuta wake ulianguka, hali iliyowalazimu kuishi bila makazi salama.

Amesema kuwa taasisi hiyo imelenga kuboresha maisha ya jamii kwa kutoa elimu ya malezi kwa watoto pamoja na kusaidia wenye mahitaji maalumu na makundi mengine yenye uhitaji.

“Lengo letu ni kujenga familia yenye elimu, afya na usawa. Katika kufikia malengo hayo, tunafanya kazi kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuleta mabadiliko chanya na maendeleo endelevu,” amesema Mbwana.

Kwa upande wake, Lupita ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo, akisema utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya makazi anayokumbana nayo.

Amesisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kuwasaidia watu wenye uhitaji ili kuboresha maisha yao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button