Muliro aionya jamii kuhusisha uhalifu na makabila
DAR ES SALAAM: Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, amewapongeza viongozi na wanajamii wa Kimasai wanaoishi jijini humo kwa kuendeleza misingi ya uaminifu, uadilifu na uwajibikaji katika shughuli mbalimbali wanazotekeleza.
Akizungumza na viongozi wa jamii hiyo, Muliro alisema ameridhishwa na namna walivyojitokeza kujadili masuala yanayozingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatua aliyosema inaendelea kuimarisha imani ya wananchi kwa jamii ya Kimasai kama kundi linaloheshimu haki na usawa.
Kamanda Muliro alisisitiza kuwa si sahihi kuwahusisha watu wote wa kabila fulani na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu. Alieleza kuwa wahalifu wanapaswa kutambulika kwa matendo yao binafsi badala ya kuhusishwa na makabila wanayotoka.
Alisema ni makosa kwa wananchi kutumia majina ya makabila kuwatambulisha wahalifu au kutoa hukumu kwa jamii nzima kutokana na matendo ya watu wachache. Kwa mujibu wake, Katiba ya Tanzania inasisitiza usawa wa wananchi wote bila kujali kabila au asili yao.
Kauli ya kamanda huyo imekuja kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanajamii wa Kimasai waliodai kukumbana na maneno ya dhihaka na lawama kutoka kwa baadhi ya wananchi baada ya tukio la kuuawa kwa muwekezaji raia wa China katika eneo la Mabibo, Dar es Salaam.
Katika tukio hilo, watu wanaodaiwa kuwa walinzi wa marehemu na wanaotajwa kutoka jamii ya Kimasai wanahusishwa na mauaji hayo, hali iliyochochea mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii na miongoni mwa wananchi.
Hata hivyo, viongozi wa jamii ya Kimasai wameendelea kusisitiza kuwa si sahihi kuwahukumu au kuwahusisha watu wote wa kabila hilo na tuhuma zinazowakabili watu wachache. Wamesema uwajibikaji wa makosa ya jinai ni wa mtu binafsi na haupaswi kuhamishiwa kwa jamii nzima.
Muliro ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuheshimu misingi ya sheria, haki na usawa, huku akisisitiza umuhimu wa kuepuka kauli zinazoweza kuibua ubaguzi au migawanyiko katika jamii.



