Bil 58/- zaokolewa Kigoma kuunganishwa gridi ya taifa

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco) Gissima Nyamo-Hanga akiwa na viongozi wengine shirika hilo wametembelea mradi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Kidahwe Kigoma (400/220/132/33kV) kujionea maendeleo ya uendeshaji wa kituo hicho baada ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa hivi karibuni.

Nyama Hanga amesema hatua hiyo imefanya Serikali kuokoa kiasi cha Sh bilioni 58.4 ambazo awali zilikuwa gharama zikitumika kwa mwaka kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli mkoani humo.
Akizungumzia juu ya kuimarika kwa huduma ya umeme, Gissima amesema kuwa huduma ya umeme katika Mkoa wa Kigoma sasa itakuwa bora zaidi kwa sababu wananchi wameanza kupata umeme kutoka gridi ya umeme ya taifa hatua ambayo inatoa fursa za kujitanua katika kuendesha shughuli mbalimbali zenye mahitaji ya matumizi ya umeme.

“Mbali na Mradi huu wa Kituo cha Kidahwe, tutaendelea na ujenzi wa Kituo kingine kikubwa zaidi chenye uwezo wa MVA 240 katika eneo hili la Kidahwe kwa ajili ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa umeme ukizingatia shughuli za kiuchumi katika Mkoa huu zinakua kwa haraka, sisi kama Shirika tukaona tuongeze mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2026,” alieleza Gissima.

Amesema kuwa, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TANESCO imejenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma kwenye Kituo cha Kidahwe yenye urefu wa kilomita 280 njia ambayo imewezesha Mkoa wa Kigoma kuungwa kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa.



