Bilioni 3/- kutekeleza afua VVU

SERIKALI inakusudia kuwekeza Sh bilioni 3.3 kwa ajili ya utekelezaji wa afua za VVU na kifua kikuu katika Mkoa wa Mtwara kwa mwaka wa fedha 2025.

Akizungumza leo mkoani wakati wa ghafla fupi ya usainishaji wa mkataba ya utoaji wa ruzuku ya mradi wa USAID Afya Yangu kwa mwaka 2025, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa USAID Afya Yangu Patrick Ngimbwa amesema ufanishi wa miradi huo kwa kiasi kikubwa unategemea usimamizi na ufatiliaji wa karibu wa viongozi wa afya kutoka ngazi zote za afya mkoani humo.

‘’Tunaomba kusimamia kwa ufanisi mkubwa utekelezaji wa shughuli zilizoainishwa katika mikataba hii ni imani yetu kwa ushirikiano wa viongozi wetu katika mkoa wa Mtwara, mradi wa Afya Yangu kanda ya kusini utatekelezwa kwa mafanikio makubwa, nitoe rai kwa viongozi wa ngazi zote pale inapotokea changamoto yoyote musisite kuwasiliana na timu yetu ya mkoa kwa ajili ya kutatua kwa pamoja changamoto itayokuwa imejitokeza,’’amesema Patrick.

Advertisement

Mkataba huo uliyosainiwa ni mwendelezo wa kile ilichofanyika kwa muda wa miaka mitatu mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuongeza mahitaji na matumizi ya huduma jumuishi na bora za kupambana na virusi vya ukimwi, kifua kikuu na kukuza tabia chanya kwa watanzania ya kujali afya yao.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkowa wa Mtwara, Nanjiva Nzunda amesema mradi wa USAID Afya Yangu kanda ya kusini ni wa miaka mitano kuanzia Oktoba 2021 mpaka Septemba 2026 unaofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia shirika la maendeleo la kimataifa la USAID.

Amesema mradi uko katika mwaka wa nne wa utekelezaji na umekuwa ukifanya vizuri na mpaka sasa jumla ya wagonjwa 33,278 elfu sawa na asilimia 97.4 kati ya wagonjwa 34,149 elfu wamesajiliwa kwa alama ya vidole, Lengo ni kuhakikisha mkoa huo hauna wagonjwa hewa hivyo kusaidia serikali kufanya maoteo sahihi ya dawa na vitendanishi kwa ajili ya watu wanaoishi na VVU.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amepongeza uwepo wa mradi huo wenye lengo la kushirikiana na serikali yao kutoa huduma bora na jumuishi za mafunzo, tiba na kuzuia maambukizi ya VVU na kifua kikuu hususani kwa vijana na watoto katika mikoa sita nchini ikiwemo mkoa wa Mtwara.

‘’Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na mradi wa USAID Afya Yangu na wadau wengine imepiga hatua kubwa katika kutoa elimu juu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi kuibua watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na kuwaanzishia dawa za kuongeza muda na kupunguza makali ya virusi vya ukimwi’’amesema Sawala

Hadi kufikia Septemba 2024 zaidi ya watu 100,000 wamepimwa na kujua hali zao za maambukizi ya VVU ambapo kati yao watu 2,955 elfu wamegundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo na kuanzishiwa dawa za ARV ambapo hadi sasa mkoa una zaidi ya watu 35 elfu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU.