Biteko ahimiza mshikamano, upendo, umoja Msalala

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kuwa angependa kuona wananchi wa Kahama wanashirikiana na kuungana kwa pamoja katika shughuli za maendeleo ya Wilaya yao.
Aidha, amewaasa kutoacha msingi wa Chama Cha Mapinduzi wa kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba Taifa linategemea CCM iwahudumie na sio kuruhusu mipasuko miongoni mwao.

Dk Biteko ameyasema hayo Kahama, mkoani Shinyanga wakati aliposhiriki katika Mkutano Maalum wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Msalala uliolenga kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025.
Akizungumzia fursa za maendeleo zilizopo wilayani humo, Dk Biteko amesema kuwa Kahama ni Wilaya ya kimkakati ambayo ina bandari kavu iliyopo Isaka ambapo pia kitajengwa kiwanda cha kuchenjua madini pamoja na uwepo wa barabara inayoounganisha nchi za maziwa makuu.
“Kutokana na uwepo wa fursa hizi tukishindwa kuungana tukashughulika na maendeeo ya watu basi watatushangaa. Nataka nitoe wito, pendaneni, shikamaneni Mungu amewapa kila aina ya utajiri tumieni fursa hiyo kujiletea maendeleo kwenye wilaya yenu na msiruhusu mipasuko katika chama chetu,” amesema Dk Biteko.

Amesisitiza: “Nawaomba baada ya mkutano huu tutoke hapa tukiwa wamoja na tuweke mbele maslahi ya Chama chetu na watu wetu,”
Pia, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Msalala, kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha wananchi wa Jimbo hilo wanapata miradi ya maendeleo na hivyo kutatua changamoto walizokuwa nazo hapo awali.
Katika hatua nyingine, Dk Biteko amemshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika Jimbo hilo ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali kama vile ya maji, elimu, afya na miundombinu.



