DODOMA – NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka watendaji waanze kujiandaa kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutafuta vyanzo mbalimbali, kwani pamoja na mitambo kuingiza umeme katika gridi ya taifa, mahitaji yanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Amesema itafika wakati umeme huo utakuwa hautoshi, hivyo ni wajibu kuanza kutafutia ufumbuzi changamoto hiyo. Dk Biteko aliyasema hayo wakati akizindua Taarifa za Utendaji katika Sekta ya Nishati kwa mwaka 2022/23.
Alisema sekta ya nishati imepata mafanikio lakini kwa kiasi kikubwa yamebebwa na sekta ya umeme kwani hivi sasa kuna umeme wa uhakika nchini hata kama changamoto iliyobaki ni miundombinu.
Aidha, alipongeza mchango wa sekta binafsi katika kuleta mafanikio katika sekta ya nishati lakini akaitaka kuendelea kuchangamkia fursa nyingi zilizopo katika sekta hiyo.
SOMA: Biteko azindua taarifa za Nishati
Pia, ameziagiza taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo na Ofisi ya Rais Mipango kuhakikisha wanasoma taarifa hizo za utendaji za mwaka 2022/23 za sekta ndogo ya umeme, gesi na petroli, kuzichambua na kutafuta changamoto na zitafutiwe ufumbuzi ndani ya miezi mitatu.
Alisema sekta binafsi imetoa mchango katika kutekeleza miradi akatoa mfano wa umeme ulipokuwa umefikia megawati 1,911, sekta binafsi ilichangia megawati 222.
Aliwataka pia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) watumie utaratibu huo kutoa taarifa za maji pia katika taarifa za mwakani kuwe na ukurasa kuhusu nishati safi na utaratibu wake wa kushughulikia.
Mwakilishi wa Kamati ya Nishati, Dk Angelina Mabula aliwataka Ewura kuendelea kutoa elimu kwa umma kujua katika ankara zinazotolewa mfano za maji makato kwenye risiti yanayohusu mamlaka hayo wajue.