Tubadili mtindo wa maisha kuzuia vifo

DODOMA : SERIKALI imesema asilimia 80 ya vifo nchini vinaweza kuzuilika kama Watanzania wataamua kubadili mtindo wa maisha.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema hayo Dodoma jana alipomwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kilele cha msimu wa sita wa mbio za NBC Dodoma kukusanya fedha kwa ajili ya kuokoa afya ya mama na mtoto.
“Taarifa ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2022 inaeleza kuwa mazoezi ya mara kwa mara kama vile kukimbia, yana uwezo wa kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo kwa zaidi ya asilimia 35. Vile vile, mazoezi ya mwili husaidia kujikinga na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa mengine mengi,” alisema Dk Biteko.
Amesema asilimia 33 ya Watanzania watu wazima wana uzito uliopitiliza na asilimia 28 wana shinikizo la damu. Dk Biteko alisema magonjwa hayo yanachangia zaidi ya asilimia 40 ya vifo vya mapema lakini asilimia 80 ya vifo hivyo vinaweza kuzuilika kwa kubadili mtindo wa maisha.
Pia ameipongeza Benki ya NBC kupitia mbio za NBC Dodoma kwa kuiunga mkono serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya kwa kuwa mwaka huu mbio hizo zimelenga kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Amesema , mbio hizo zimelenga kufadhili wa masomo ya wakunga kupitia Taasisi ya Benjamin Mkapa ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi na kutoa ufadhili kwa mafunzo ya wauguzi maalumu wa kusaidia watoto wenye changamoto ya usonji kwa kushirikiana na AMREF Afrika.
Dk Biteko amesema tangu kuanzishwa mbio za NBC Dodoma kwaka 2020 imekuwa ni moja ya vielelezo vya kujenga mshikamano, uzalendo wa kweli na kutatua matatizo katika jamii zikiwemo changamoto za kiafya. SOMA: Makamu wa Pili wa Rais SMZ ahimiza mazoezi
Alipongeza mbio za NBC Dodoma kwa kuendelea kuimarika kwa kuwa mwaka 2024 zilihusisha washiriki 8,000 na mwaka huu zimekuwa na washiriki zaidi ya 12,000 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 50. Vilevile mwaka jana mbio hizo zilikusanya Sh milioni 300 na mwaka huu zimekusanywa Sh milioni 700 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 133.33.
Dk Biteko alihimiza Wizara ya Afya, serikali za mitaa, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wananchi wote wafanye mazoezi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ili kujikinga na matatizo ya afya. “Nitashukuru sana kusikia kila taasisi imetenga kwa uchache siku moja kwa mwezi wa ajili ya kufanya mazoezi ya pamoja, hii itasaidia kuimarisha afya zetu na kujenga Taifa imara,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema NBC Marathon imekuwa ni moja ya alama za sekta binafsi katika kuwekeza kwenye sekta ya afya na nyinginezo. Sabi amesema katika kipindi cha miaka mitano mbio hizo zimekusanya zaidi ya Sh bilioni moja ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya afya.
Aliongezea kuwa, mbio hizo zimechangia ujenzi wa wodi ya wanawake katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam na maeneo mengine katika maendeleo ya sekta ya afya. Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema mbio za NBC Dodoma zimekuwa kivutio kwa wanamichezo na akasema wizara hiyo itaendelea kuiunga mkono benki ya NBC katika maandalizi ya mbio hizo.