Biteko: Tujenge mazingira kuepusha migogoro baada ya vifo
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka wanajamii wajiepushe na mazingira yanayoweza kusababisha migogoro baada ya wao kufariki dunia.
Amesema hayo Dar es Salaam alipomwakilisha, Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA).
Alisema wanajamii wakijiandaa na kuweka mazingira mazuri, wataepusha migogoro isiyo ya lazima na jamii itaishi kwa amani na kupunguza gharama zinazotumika kurekebisha jamii yenye migogoro.
Aidha, ameipongeza Tawla kwa kazi nzuri iliyodumu kwa miaka 35 tangu kuazishwa kwake mwaka 1990.
Dk Biteko aliwasilisha pongezi za Rais Samia kwa Tawla kupitia kushiriki Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Alisema serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha jamii inaishi kwa amani na upendo kama ilivyo ndoto ya Tawla ya kuwasaidia watu wenye uhitaji.
Dk Biteko ameutaka uongozi wa Tawla kuendelea kuwashawishi na kuwavutia wanachama wapya watakaoweza kutoa msaada bila kusita katika jamii yao.
Alisema serikali imechukua hatua kuhakikisha wanawake wanakuwa katika nafasi za uamuzi kwa kuongeza uwiano wa majaji wanawake na wanaume katika mahakama za rufani na mahakama kuu.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu ujao, Dk Biteko alihimiza wajumbe wenye nia wajitokeze kugombea uongozi ili kuwakilisha wananchi hususani wanawake wanaongezeka. Mwenyekiti wa Tawla,
Suzan Ndomba ameipongeza serikali kwa hatua za kulinda haki na kushughulikia changamoto za zinazowakabili wanawake na watoto nchini.
Suzan alisema hatua ya serikali kuwekeza katika utekelezaji wa miradi ya nishati, maji na elimu ni fursa kwa kundi la wanawake wa Tanzania ambao wamekuwa waathirika wakubwa madhara yanayotokana na ukosefu wa
miundombinu hiyo.



