Bodaboda wanaswa wizi wa diseli Morogoro

POLISI mkoani Morogoro inawashikilia vijana wawili madereva wa bodaboda kwa tuhuma za kusafirisha madumu 19 ya mafuta ya dizeli yenye ujazo wa lita 20 wanayoyaiba kwenye mradi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kutokea Kiberege – Ifakara mjini wilayani Kilombero.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema hayo Februari 3, 2024 kuwa kukamatwa kwa watu hao kulitokana na misako na operesheni zinazoendelea maeneo mbalimbali mkoani humo.

Mkama ,amewataja waliokamatwa ni Yusuph Rashid (34) mkulima na dereva wa bodaboda mkazi wa Ruaha na mwenzake Edmond Sengelele (32) mkulima na dereva wa bodaboda pia mkazi wa Ruaha , Tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero.

Advertisement

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na madumu 19 ya mafuta ya dizeli yenye ujazo wa lita 20 ambapo jumla walikutwa na lita 380 wakiwa wameyabeba kwenye pikipiki mbili zenye usajili wa namba MC 534 DNU na MC 154 CVV aina ya Houjue.

“ Baada ya mahojiano ya awali imebainika kuwa mafuta hayo wanayaiba kwenye mradi wa barabara inayojengwa kutokea Kiberege mpaka Ifakara “amesema Mkama .

Kamanda wa Polisi wa mkoa huyo amesema mahojiano zaidi yanaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.