Bodi TEMDO yatakiwa kutengeneza fedha

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Suleimani Jafo ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) kuhakikisha inatengeneza misingi sahihi ya upatikanaji fedha ili kutimiza malengo ya taasisi hiyo katika kukuza wa uchumi wa viwanda.
Dk Jafo amesema hayo jijini Arusha wakati wa uzinduzi bodi hiyo uliofanyika katika taasisi hiyo.

Amesema wizara yake itashirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuhakikisha taasisi za umma zinanunua vifaa tiba vinvyotengenezwa na TEMDO ili kuokoa fedha nyingi inayotumika kuagiza vifaa hivyo nje ya nchi.
Vilevile ameishauri bodi hiyo kushirikiana na taasisi nyingine kama vile Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) na nyinginezo ili kupata fedha za kuendeleza miradi mbalimbali itakayoanzishwa katika taasisi hizo.

Katika hatua nyingine amewasihi wajumbe hao wa bodi pamoja na watumishi wa TEMDO kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, ubunifu na upendo ili kuleta tija na ufanisi katika utendaji kazi na utoaji huduma kwa ummakutimiza malengo ya Taasisi hiyo katika kuleta taswira nzuri ya kuhakikisha maendeleo ya TEMDO yanakuwa.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk, Hashil Abdallah amesisitiza bodi hiyo kuhakikisha maendeleo ya viwanda yanakua ikiwemo utekelezaji wa sera sanjari na kubuni miradi mbalimbali.

Wakati huo huo,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Temdo, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia amesema bodi hiyo itafanya kazi kwa bidii katika kukuza maendeleo ikiwemo kubuni miradi yenye kuleta mapinduzi katika sekta ya viwanda.



