Bodi ya Ithibati yaanza kung’ata

DAR ES SALAAM; Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imewapiga marufuku watangazaji wanne kujihusuisha na masuala ya kihabari wakidaiwa kukiuka sheria na maadili ya taaluma ya habari.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Patrick Kipangula, imesema kuwa uamuzi huo umeanza leo Julai 18, 2025 mpaka hapo watakapotimiza matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na sifa za kielimu na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.
Watangazaji hao wa kituo cha redio cha Mjini FM ni Deodatha William, Mussa Crispin Mgenge, Perfect Crispin na Iddy Bakari Iddy, inaelezwa kupitia kipindi chao walifanya mahojiano na msanii wa singeli Dogo Pateni.
Hata hivyo Bodi imesema maudhui ya kipindi hicho yalihitaji uchambuzi wa kina, hivyo leo watangazaji hao waliitwa kupata ufafanuzi.
“Baada ya kufanya mahojiano na tathmini ya kitaalamu kuhusu maudhui ya kipindi hicho, Bodi imebaini kuwa;
“Watangazaji hao hawajasajiliwa na kupewa Ithibati na Bodi, hivyo wanafanya kazi za kihabari kinyume na Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023);
“Watangazaji hao walikiuka haki ya faragha na kutweza utu wa mhojiwa kwa kumlazimisha kutoa taarifa binafsi bila ridhaa yake kinyume na Kanuni ya 11(1)(e) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji ya Redio na Televisheni), 2018 (kama zilivyofanyiwa marekebisho); na
“Watangazaji hao walitumia lugha ya kumshushia hadhi mhojiwa kinyume na Kanuni ya 11(1)(f) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji ya Redio na Televisheni), 2018 (kama zilivyofanyiwa marekebisho) na Kanuni ya 16(1), ikisomwa pamoja na Jedwali la Tatu aya ya 2(b) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2020.
“Kutokana na ukiukwaji huo mkubwa wa Sheria na maadili ya taaluma ya habari, Bodi imewapiga marufuku watangazaji tajwa hapo juu kujihusisha na masuala ya kihabari kuanzia tarehe 18 Julai, 2025 mpaka hapo watakapotimiza matakwa ya Sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na sifa za kielimu na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari,” imesema taarifa hiyo.



