MOROGORO: BODI ya Maji Bonde la Wami-Ruvu imeendelea kuchukua hatua stahiki kwa kupanda miti milioni mbili kwa kila Mkoa unaosimamiwa na bonde hilo ambao ni mkakati maalumu wa uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwemo eneo la Bwawa la Mindu , Manispaa ya Morogoro ukiwa ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Dk Philip Isdory Mpango .
Kaimu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira, Dauson Rwamihago amesema hayo kwenye taarifa yake Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira katika Bwawa la Mindu kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024, Godfrey Mnzava.
Rwamihago amesema mradi huo umegharimu zaidi ya Sh milioni 50 ambazo ni michango ya miche na nguvu kazi ya jamii ikiwa na lengo la kulinda chanzo hicho cha maji kinachotegemewa na kwa zaidi ya asilimia 70 na wakazi wa Manispaa ya Morogoro.
Mradi huu umelenga kusaidia upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro, kuongeza kiwango cha uhifadhi wa Mazingira na ulinzi wa vyanzo vya maji na kuoongezeka uhifadhi wa ikolojia.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Mnzava alipongeza hatua madhubuti zinazochukuliwa na Bodi ya Bonde la Wami Ruvu katika kutunza vyanzo vya maji kwa kuendelea kuhamasisha zoezi la upandaji wa miti ambapo mpaka sasa takribani miti 24,255 imekwisha pandwa chini ya mradi huo.
“Hata kwa kuangalia inaonesha watu wapo Serious (Makini) kwenye upandaji wa miti katika chanzo hiki cha maji, na tumeona kuona miti iliyopandwa katika Mwenge wa uhuru 2023 na namna ambavyo inaendelea,” amesema Mnzava.
“… Mlipanda miti 2,000 na miti 1, 939 inaendelea vizuri, wenzetu wa Wami wanaendelea kurudishia miti 61 ambayo imekufa nah ii kazi mmeifanya vizuri kwenye eneo la utunzaji wa mazingira na upandaji miti, Bodi ya maji Wami Ruvu hatuwadai chochote’ amesisitiza Mnzava.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa alitumia fursa hiyo kuwapongeza Wananchi wa Manispaa ya Morogoro na Kikosi cha Jeshi la Mzinga kwa kuungana na Serikali katika ulinzi na utunzaji wa mazingira katika Maeneo mbalimbali ya vyanzo vya maji.
Nsemwa alisema mpaka sasa miti 76,926 imepandwa katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya hiyo yakiwemo ya shule, hifadhi ya Milima Ulunguru, Bwawa la Mindu pamoja na eneo la Jeshi la Magadu.
Kwa mijibu wa taarifa ya Bonde la Wami Ruvu, kuwa linajuuisha sehemu za mikoa ya Dodoma, Manyara, Morogoro, Pwani, Tanga na mkoa wote wa Dar es Salaam likiwa na jumla ya wilaya 22 za mikoa hiyo.
Bonde linakadiriwa kuwa na kilometa za mraba 66,820 huku eneo la mto Wami likiwa na kilometa za mraba 43,946 na eneo la mto Ruvu likiwa na kilometa za mraba 18,078 na eneo la bonde la mito ya Mpiji, Mlalakuwa, Msimbazi, Kizinga, Mzinga na Mbezi ikiwa na kilometa za mraba 4,796.