DAR-ES-SALAAM: BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema ina wajibu wa kuikopesha serikali mkopo wa muda mfupi usio wa kibajeti wa asilimia 18 na kwamba serikali imekuwa ikilipa madeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki BoT, Agathon Kipandula alisema mkopo wanaotoa kwa serikali upo kwa mujibu wa Sheria Sura ya 197 ya Mwaka 2006.
Kipandula alisema utaratibu unaofanyika ni kwa benki kuu zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani kwani wote wanatumia sheria moja.
SOMA:Mwigulu: Hakuna uchotaji fedha BoT
Kwa mujibu wa sheria benki kuu imepewa mamlaka ya kutunza fedha za serikali zote mbili na mashirika ya umma, hivyo pale wanapokuwa na uhitaji huwakopesha.
Alieleza kuwa kwa sababu ya kuwa na mteja ambaye ni serikali, sheria hiyo imetoa nafasi ya kutoa mkopo wa muda mfupi kwa lengo la kurekebisha kushuka na kupanda kwa mapato ya serikali.
“Sheria hii pia imeweka ukomo wa kukopa ambao kwa mujibu wa sheria ni asilimia 18 ya mapato ya mwaka jana,” alifafanua Kipandula.
Aliongeza kuwa: “Kwa mambo ambayo yanaendelea, sheria inatusimamia katika kuendesha shughuli za serikali ikiwemo kutoa huduma ya mkopo wa muda mfupi kuziba pengo au nakisi”.
Kipandula alisema sheria hiyo inaitaka serikali kuchukua mkopo huo usio wa bajeti ndani ya siku 180 na kwamba kila mwisho wa mwezi serikali inarudi katika nafasi yake na kurejesha mkopo huo.
“Mkopo huu sio ule ambao tuna-determine amount kwamba watakopa kiasi hiki, huu una-balance cash flow yake kwamba kama leo ana jukumu la kulipa Sh 10,000 na alizo nazo ni Sh 5,000, basi Sh 10,000 itakuja kama overdraft na akipata fedha zake basi atarudisha,” alisema Kipandula.
Alisisitiza si kweli kuwa serikali ilikopeshwa kiasi cha fedha na BoT kwa aina tofauti kwani hata kwenye vitabu vya serikali hakuna kiasi hicho. Aidha, alisema mkopo wa aina hiyo hauhitaji kupitishwa na Bunge isipokuwa wataonesha kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Kulikuwa na taarifa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Fedha ameshalitolea ufafanuzi, tunachokieleza hapa ni kuongeza uelewa wa masuala yanayoendelea BoT,’’ alisema Kipandula.
SOMA: https://www.bot.go.tz/?lang=sw
Juzi Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alieleza kuwa hakuna utata au uchotaji wa fedha BoT.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X, Dk Mwigulu alieleza kuwa BoT inasimamia kwa umakini sheria za nchi na miiko ya benki kuu zote duniani.
BoT inasimamia kwa umakini sheria za nchi na miiko ya benki kuu zote duniani. Dk Mwigulu alieleza kuwa Sheria ya BoT inaruhusu kutoa mikopo ya muda mfupi kwa serikali ili kukidhi mahitaji ya matumizi ambayo yanakuwa hayajapata mapato.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 34 hadi 37 cha BoT Act, Serikali inaruhusiwa kukopa hadi 18% ya makusanyo halisi ya ndani ya mwaka uliopita” alieleza Dk Mwigulu. Aliongeza: “Hili limekuwa likifanyika hivyo tangu BoT ianzishwe.
BoT ni benki ya serikali, serikali huchukua advance kwa mujibu wa sheria badala ya kukopa kwa riba kubwa kutoka benki za kibiashara”. Dk Mwigulu alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/23, serikali ilikuwa inaweza kukopa BoT kiasi kinachofikia Sh trilioni 4.5.
Alieleza kuwa taarifa ya kuwepo kwa mkopo wa Sh trilioni 1.7 ni suala ambalo liko ndani ya wigo unaokubalika kisheria.