BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza kununua madini ya dhahabu ili iwepo akiba ya madini hayo nchini na tayari imeshanunua kilo 400. Hayo yalibainishwa na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko wakati akihitimisha hoja ya hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2023/24 bungeni Dodoma jana ambapo Bunge lilipitisha bajeti yake ya Sh bilioni 89.4.
Dk Biteko alisema katika mabadiliko ya Sheria ya Madini mwaka 2017, Bunge lilielekeza kuwa madini yote yaongezwe thamani hapa nchini. Alisema kutokana na hilo, kazi ya kwanza ilikuwa kuwavutia watu kuja kujenga mitambo ya kusafishia dhahabu, lakini ili kupata cheti cha mtambo wa kusafishia dhahabu, huchukua muda mrefu.
Kwa mujibu wa Dk Biteko, wapo watu waliofikia hatua ya kupata cheti cha Shirika la Viwango vya kimataifa (ISO) na wengine wanakamilisha taratibu ili kazi hiyo ianze kufanyika. “Tulichoamua na Benki Kuu walikuja kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ya Dunstan Kitandula, wakatoa taarifa kuwa kanuni ya kununua dhahabu tayari imekamilika na wameanza kununua dhahabu na hivi ninavyozungumza wameshanunua kilo 400.
“Tunachotaka sasa, tunakamilisha taratibu zilizopo kwenye mitambo ya kusafishia dhahabu ili tuweze kuanza kununua dhahabu kama serikali na tuanzishe hifadhi ya dhahabu nchini, tutaenda taratibu lakini tunataka twende kwa uhakika ili makosa yaliyojitokeza huko nyuma yasijirudie,” alisema.