BoT yaonya hatari ya fedha mtandaoni

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema fedha za mtandaoni ni hatari. Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba amesema fedha hizo hazitambuliki zina vihatarishi vingi kuliko faida na hazina njia za kuzidhibiti. Tutuba amesema hayo ofisini kwake Dodoma wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha Kasri la Kikeke kilichorushwa na kituo cha habari cha Crown.

“Nawashauri wananchi, hasa vijana wasiende kuwekeza kwenye maeneo kama hayo kwa sababu yana hatari kubwa. Pia, wajitafutie maeneo sahihi na salama ya uwekezaji, wafuatilie na kujielimisha kuhusu matumizi sahihi ya fedha,” alieleza Gavana wa Benki Kuu.

Amesema mtu akiwekeza kwenye fedha mtandao, anaweza akamtafuta mtu anayetoa fedha na asimpate kwa sababu mifumo ya uendeshaji uchumi wao si rasmi. Amesema pia anaweza akaweka fedha kununua Shilingi lakini baada ya kufanya malipo, asiikute tena na akawa ametapeliwa bila ya kuwa na mtu wa kumdai.

Tutuba amesema watu wanawekeza kwenye fedha mtandao kwa sababu hawana elimu ya usahihi wa fedha mtandao, lakini pia wanapaswa kutambua hakuna mifumo rasmi ya kufuatilia na kudhibiti, na mitandao hiyo haijathibitishwa kwenye mifuko ya kulinda thamani ya fedha hizo.

“Tunawasihi watu wasiwekeze kwenye fedha mtandao. Tumeshafanya tathmini na tumeunda timu ya wataalamu ya udhibiti na usimamizi wa fedha hizo, tumeshandaa mwongozo na sheria itakuja ya namna ya kusimamia na kudhibiti fedha hizo ili itakapotokea hatari mbalimbali, waweze kushughulika nazo,” alieleza.

Ameeleza mwaka 2023 walifanya tathmini na kutambua kiwango cha elimu ya fedha kipo chini, ndipo walipokuja na mitaala miwili ambayo ni ya elimu ya fedha ndani ya mifumo rasmi ya elimu na usio wa mifumo rasmi wa elimu ya shule. SOMA: BoT mbioni kuvuka lengo ununuzi dhahabu

Amesema katika mitaala hiyo wanaelimishwa namna ya kuweka akiba na maeneo mbalimbali ya uwekezaji pamoja na namna ya kuzitawala fedha. Kuhusu kiwango cha riba ya mikopo inayotolewa benki, alisema riba inapoenda kwa mtu ina vigezo mbalimbali kwa sababu benki inatafuta fedha kutoka kwenye vyanzo tofauti, ikiwamo kwenye amana na kukopa ndani kupitia ushirikiano baina ya benki ambazo kwa mwaka zinakwenda hadi asilimia 10 mpaka 15.

“Tunatumia mifumo ya soko kwenye usimamizi wa riba hizo ambazo zinakwenda sambamba kanuni, na ili kulingana na huo ukomo tulitengeneza dirisha maalumu na kuwapunguzia baadhi ya riba ili wapate fedha za kwenda kukopesha na tuliwapata sharti la kwamba lazima riba iwe chini na hawajaweka kiwango cha benki kuwa na riba maalumu kwa mteja,” alifafanua.

Kuhusu madai ya BoT kuipa fedha serikali kukamilisha miradi ya maendeleo, alisema serikali inapata fedha BoT kupitia gawio kwa sababu benki hiyo inafanya biashara na inapata faida ya uwekezaji serikali inayofanya kupitia akaunti zake hivyo fedha hizo zikitumika katika miradi ya maendeleo ni jambo la kawaida.

“Benki Kuu ni benki ya serikali ndio maana tuna akaunti za serikali na akaunti za benki zote nchini na kuna ukomo uliowekwa wa kupeleka fedha serikalini, sheria inataka asilimia 18 ya mapato yaliyopatikana kwa mwaka wa fedha ndio yapelekwe kwa serikali,” alibainisha. Tutuba amesema  eneo lingine la serikali kupata fedha BoT ni kuuza hatifungani na dhamana za serikali na ndio maana kila Jumatatu kunakuwa na minada.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button