TRA: Ole wenu mnaokwepa kodi
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeonya wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi, ikisema watawagundua na kupata hasara zaidi.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alitoa onyo hilo akizindua Kituo cha Huduma kwa Walipakodi Masaki katika Mkoa wa Kikodi Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
“Katika vitu ambavyo havifutiki ni kodi, isipokuwa kwa kulipa ama kama kutakuwa na kesi mahakamani ikaamua vinginevyo, nje ya hapo utadanganywa, ukidanganywa baadaye tutakugundua, tukikugundua utapata gharama mara mbili, utalipa kodi yenyewe utalipa na riba,” alifafanua Mwenda.
Aliongeza: “Kama una jambo lolote njoo ofisini na ndio maana tunaweka huduma karibu ili tuweze kukushauri lakini sio kuonana na watu wa mtaani watakupa ushauri, haitawezekana sana sana utapata tu maradhi ya moyo… Sasa ili wasipate ugonjwa wa moyo walipe kodi zao kwa wakati na wasikubali kudanganywa.”
Aidha, alizungumzia Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS) unaofanya kazi saa 24, akisema huo ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali unaoondoa gharama kwa walipakodi, hivyo ni vema wakautumia.
Mwenda alisema lengo la kuanzishwa mfumo huo ni kuwa na mfumo mmoja jumuishi utakaosaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi na kulinda haki za walipakodi na utasaidia katika utunzaji wa kumbukumbu.
Mfumo huo unajumuisha huduma zote zilizokuwa zinatolewa katika mifumo ya TRA ikiwamo usajili wa walipakodi, utumiaji wa taarifa zote za kodi, ulipaji wa kodi, mawasiliano na madai mbalimbali. Pia, mfumo huo umeungana na mfumo wa forodha ambao utaonesha kilichouzwa, kilichobaki na mapato yaliyopatikana.
“Kupitia mfumo huu hakuna mlipakodi atakayeonewa… Huu ni uwekezaji mkubwa ambao serikali imeweka kuanzisha mfumo unaoondoa gharama na unaotenda haki na Masaki na Osterbay itakuwa eneo la kujifunza kutoa risiti kwa usahihi kwa mfumo huo,” alisema Mwenda.
Aidha, aliwataka wanaofanya biashara ya nyumba na viwanja kuwa makini katika ulipaji kodi, kwani kwa siku za karibuni kumekuwa na malalamiko mengi juu ya wafanyabishara hiyo.
Akizungumzia kituo hicho, Mwenda asliema Masaki ni eneo muhimu kwa sababu ni mahali pekee nchini viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wanaishi kwa wingi.
“Lakini Masaki ni eneo la watu wenye kipato cha kati na cha juu wanaishi na kufanya shughuli zao huku,” alisema.
Aliongeza: “Tunaanzisha kituo hiki kwa sababu tumeagizwa kuimarisha na kuongeza huduma kwa walipakodi, badala ya kwenda kituo cha Sam Nujoma au Millennium Tower sasa watahudumiwa hapa… Kituo hiki kitafanya huduma zote ikiwemo kusajili walipakodi, kutoa elimu na ushauri.”



