HATUA za kujenga boti moja ya matibabu na mbili za utafutaji na uokoaji zitakazotumika katika Ziwa Victoria zimekamilika baada ya kumpata mzabuni.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo bungeni ikiwa ni miongoni mwa mafanikio ya mwaka 2022/23.
Profesa Mbarawa amesema mafanikio hayo yametokana na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC ), katika kusimamia vyema udhibiti wa huduma za usafiri.
Amesema kwa sasa taarifa ya Uchambuzi wa zabuni imewasilishwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
“Katika kusimamia vyema Udhibiti wa Huduma za Usafiri kwa njia ya Maji TASAC imeshamkabidhi Mkandarasi eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Uratibu wa shughuli za Utafutaji na Uokoaji cha kikanda kitakachojengwa eneo la Ilemela Mwanza,” amesema.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha Bungeni mpango wa Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/24 ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mbarawa amesema TASA inaendelea pia na mchakato wa kuanza ujenzi wa vituo vidogo vitatu vwa utafutaji na uokoaji.
“Mkandarasi amepatikana kwa ajili ya kujenga vituo vingine vidogo vitatu vya Utafutaji na Uokoaji katika maeneo ya Kanyala – Geita, Nansio – Ukerewe na Musoma – Mara na sasa amekabidhiwa maeneo ya ujenzi na anaendelea na maandalizi ya awali,” amesema.
Kazi ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Uratibu wa shughuli za Utafutaji na Uokoaji itakamilika ndani ya miezi 18 na Kituo cha Utafutaji Kanyala – Geita, Nansio – Ukerewe na Musoma – Mara inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12.