Bukoba Vijijini wapanda miti 500 ya matunda

HALMASHAURI ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera imeadhimisha siku ya mazingira duniani kwa kupanda miti mia tano ya matunda katika Hospitali ya Wilaya.
Akizungumza wakati wa tukio hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Dr Kisanga Makigo amehimiza taasisi na watu binafsi kuendelea kupanda miti ili kuhifadhi mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Tumeamua kuchagua eneo hili la hospitali kwani lina uhitaji wa miti ya vivuli na matunda ili kuleta mwonekano na uboreshaji wa mazingira haya yanayotoa huduma za afya lakini tunaamini kuwa hata baadhi ya miti iliyopandwa itakuwa msaada mkubwa katika kulinda mazingira yetu lakini pia itasaidia jamii inayowazunguka kupata matunda,”alisema Makigo.
Afisa mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Dominic Ruta, amesema miti hiyo ya matunda iliyopandwa ni pamoja na miparachichi, michenza na miti ya kivuli.
Amesisitiza kuwa upandaji miti huo ni endelevu katika taasisi zote za serikali na binafsi katika kuhakikisha miti inapandwa kwa wingi kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na lishe.

Amesema Halmashauri hiyo kupitia idara ya mazingira itaendelea kusambaza miti mingine aina tofauti hadi ngazi ya kaya ili kujenga jamii bora inayoendana na kulinda mazingira ambapo pia watoto wameshiriki.
Muuguzi Mkuu wa hospitali ya wilaya, Elizeus Ezra ameishukuru Halmashauri kwa kuchagua kupanda miti katika hospitali ya wilaya ambayo ni mpya kwani watumishi na wagonjwa watanufaika kwa kupata matunda na kuweka madhari nzuri ya hospitali hiyo.
Aidha amewashukuru wadau wote wa afya wa Bukoba vijijini na nje ya Bukoba wanaoendeleza juhudu za kuboresha mazingira hospitalini hapo akiahidi kuwa miti hiyo itatunzwa kama kumbukumbu bora ya siku ya mazingira Duniani ya mwaka huu.
Siku ya mazingira Duniani huadhimishwa Juni,05 kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu, “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo,Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki”.



