Bukombe yapokea mitungi ya gesi ya ruzuku 1,600

BAADHI ya wakazi wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamepokea mitungi ya gesi ya kupikia 1,600 inayouzwa kwa bei ya ruzuku ili kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu na nishati mbadala.

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, Advera Mwijage amesema hayo katika siku maalum ya nishati safi ya kupikia wilayani Bukombe iliyoratibiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Advera amesema mpaka sasa katika awamu ya kwanza ya program hiyo, REA imesambaza mitungi ya gesi zaidi ya 85,000 nchi nzima ambayo ipo tayari inatumiwa na wananchi.

“Sasa hivi tupo kwenye awamu ya pili ya usambazaji wa mitungi ya gesi ambapo tutasambaza mitungi ya gesi 452,445 na mitungi hii itasambazwa katika mikoa yote nchini.

“Kwa maana kwamba kila wilaya itapata mitungi 3,225 mradi umekwisha kuanza ambapo wasambazaji wa mitungi hii wameshaanza, amesema na kuongeza;

SOMA: Rais Samia atoa maelekezo nishati safi ya kupikia

“Lakini kwa majiko banifu tumekwisha kusambaza majiko 4,200 na tupo hatua za mwisho za kusambaza majiko zaidi ya laki mbili kwenye maeneo ya vijijini,” amesema.

Amesema bajeti ya mradi mzima wa majiko ya gesi ambao unakwenda kwenye mikoa 26 ni sh bilioni 8.6 na inatarajiwa kuongezeka kwa awamu zinazokuja kutokana na mwitikio na mapokeo.

Mratibu wa Nishati Safi ya Kupikia Wizara ya Nishati, Ngereja Mgejwa amesema dhamira kubwa ni kupambana na chanangamoto za kiafya, mazingira na kiuchumi zitokanazo na nishati chafu.

Amesema takwimu zinaonyesha mpaka sasa watu 33,000 wanafariki kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia huku lengo ni kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati salama ifikiapo 2034.

Amekiri dhana potofu juu ya matumizi ya nishati jadidifu kwa baadhi ya watu kuamini kuwa chakula kinachopikwa kwenye nishati jadidifu siyo kizuri imekuwa kikwazo lakini elimu inaendelea kutolewa.

Awali Mkuu wa wilaya ya Bukombe, Pasikasi Murigili amesema kampeni ya matumizi ya nishati jadidifu itasaidia kukabiliana na uharibifu wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Amesema mpaka sasa wilayani Bukombe asilimia 22 ya eneo linatumika kwa shughuli za binadamu huku asilimia 78 ni misitu ambayo imeanza kuvamiwa na binadamu ili kupata nishati ya kuni na mkaa.

Habari Zifananazo

Back to top button