Bunge lampongeza Samia mkutano wa nishati Dar

Rais Samia Suluhu Hassan

BUNGE limepitisha Azimio la Kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati Afrika (Misheni 300) hapa nchini.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alitangaza rasmi kwamba Bunge limepitisha azimio hilo baada ya kuwahoji wabunge wote kwa umoja wao bila tofauti za kivyama walilikubali azimio hilo.

Akisoma azimio hilo mbele ya Bunge, mbunge wa Viti Maalumu, Asia Halamga (CCM) alisema bunge hilo katika mkutano wa 18, kikao cha Nne, Januari 31, 2025, linaazimia kwa dhati na kauli moja kumpongeza Rais Samia kwa kuwa mwenyeji na kufanikisha mkutano wa nishati wa Afrika wa mwaka 2025 kwa weledi na viwango vya kimataifa.

Advertisement

Pia, alisema azimio hilo linampongeza Rais Samia kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa ifikapo 2030 Watanzania wote watakuwa wamefikiwa na miundombinu ya umeme.

Alisema pia, kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa ifikapo 2030 asilimia 75 ya Watanzania watakuwa wamepata nishati safi ya kupikia na hatimaye kufikia 2034 Watanzania wote wawe wamepata nishati safi ya kupikia.

Vilevile, alisema Azimio hilo linamuunga mkono Rais Samia katika dhamira yake ya kuwapatia Watanzania wote nishati ya umeme na nishati safi ya kupikia.

Katika mkutano huo uliofanyika Januari 27 hadi 28, 2025 ulikuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi na Afrika.

Alitaja manufaa hayo kuwa ni kwa wawekezaji katika sekta ya hoteli na malazi, usafiri na usafirishaji, wauzaji wa vyakula na vinywaji, bidhaa mbalimbali na sekta ya utalii.

Kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano, alisema wafanyabiashara wametengeneza mtandao katika biashara zao kwa kufanya mazungumzo ya kibiashara pembezoni mwa Mkutano huo.

Halamga alisema kupitia mkutano huo pia, nchi imeingiza fedha za kigeni suala ambalo limeleta manufaa makubwa kwa uchumi.

Rais Samia akifungua mkutano huo alisema, “Mkutano huu unazungumzia zaidi ya nishati, ni kuhusu kuzipa nguvu familia, kuinua mamilioni ya watu kutoka kwenye umasikini na kuleta matumaini na fursa kwa vijana. Ni ahadi yetu
kuwa, mabadiliko ya kiuchumi, kukuza viwanda, kuunda ajira na kuchochea uvumbuzi Afrika.”

Wazo la kumpongeza Rais Samia, liliibuliwa na Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG) chini ya Mwenyekiti, Shally Raymond, makamu Sofia Mwakagenda na Katibu Agnes Hokororo na kujadiliwa na bunge lote na kupitishwa.

Wakichangia Azimio hilo mbunge wa Singida Mashariki, Elibariki Kingu (CCM) alisema Afrika ina watu bilioni 1.5 ambao asilimia 60 ni vijana chini ya miaka 25, hivyo mipango hiyo itasaidia kuleta ajira kwa vijana milioni 185 kupata ajira.

Naye, Mbunge wa Kuteuliwa Shamsi Vuai Nahodha (CCM), alisema Rais Samia amekuwa kinara wa kutetea masuala ya msingi kwa binadamu, ikiwemo nishati safi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Jesca Kishowa (CHADEMA) alipongeza Mkutano Mkuu wa CCM kwa kumteua, Samia kuwa mgombea pekee katika uchaguzi wa 2025 kwani umahiri na uhodari wake umeonesha kila mwanamke anaweza kuwa rais nchini.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *