Burundi yakanusha kuondoa wanajeshi wake DR Congo

SERIKALI ya Burundi imekanusha taarifa zinazodai kuwa inawaondoa wanajeshi wake kutoka Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliokuwa wameenda kulisaidia Jeshi la Congo kupambana na waasi wa M23.

Taarifa hizo zilianza kuenea baada ya vyanzo kadhaa kudai kuwa mamia ya wanajeshi wa Burundi walionekana kuondoka eneo hilo na kurejea nyumbani, hasa kutokana na kuendelea kwa mashambulizi ya waasi hao.

Msemaji wa Jeshi la Burundi alieleza kuwa taarifa hizo ni za uongo na kwamba askari wa Burundi bado wanaendelea na operesheni hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Alisisitiza kuwa wanajeshi wa Burundi wanatekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji na kuwa hakuna mabadiliko yoyote katika shughuli zao.

Aidha, waasi wa M23 wameripotiwa kuingia katika mji wa Kamanyola, ulio takribani kilometa 50 kusini mwa mji wa Bukavu, hatua inayoongeza hofu ya kuendelea kwa mapigano katika eneo hilo lenye machafuko. Hali hii inatia shaka kwa usalama wa raia na ufanisi wa juhudi za kidiplomasia kutatua mgogoro huo.

Katika juhudi za kusitisha mapigano, Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi, alikutana na Rais wa Angola, Joao Lourenco, katika mji wa Luanda, ambapo walijadili hatua zinazohitajika kuzuia kuzorota zaidi kwa hali ya usalama katika mashariki mwa Congo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button