Bwana harusi kizimbani wizi wa ractics, fedha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imempandisha kizimbani Vicent Massawe ‘bwana harusi’ kwa makosa mawili ambayo wizi wa gari lenye thamani ya shilingi milioni 15 na utapeli wa fedha Sh milioni 3.

Massawe alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Akisoma mashtaka hayo wakili wa serikali, Frank Rimoy alidai kwamba, Novemba 15, 2024, katika wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Vicent aliiba gari aina ya Toyota Ractis T 642 EGU mali ya Silvester Massawe, ambalo hapo awali aliliazima kwa ajili ya kulitumia kwenye sherehe ya harusi yake iliyofanyika Novemba 16, 2024.

Pia, katika tarehe hiyo ilidaiwa kuwa mshtakiwa alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu shilingi milioni 3 kutoka kwa Silvester Massawe. Ilidaiwa kuwa aliazima fedha hizo akiahidi kuzirudisha huku akijua si kweli.

Mshtakiwa alikana makosa yote mawili. Aidha, wakili Rimoy alidai kuwa upelelezi bado unaendelea na kesi anayoshtakiwa Massawe ina dhamana.

“Kwa kuwa makosa ya mshtakiwa ni kudhaminika, sisi hatutakuwa na pingamizi kama atakidhi vigezo vya dhamana,” alidai wakili Rimoy.

Kwa upande wake Hakimu Nyaki amesema dhamana ipo wazi kwa mshtakiwa kama atakamilisha taratibu na aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 7, 2025.

Habari Zifananazo

Back to top button