Bwawa la JNHPP lawa kivutio maonesho ya IATF2025

ALGIERS, Algeria: Mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji, umetajwa kuwa kielelezo cha ushirikiano wa Bara la Afrika wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nne ya Biashara ya Ndani ya Afrika (IATF2025) yanayofanyika jijini Algiers.
Viongozi na maofisa waliokusanyika katika maonesho hayo ya wiki moja wanasema mradi huo wa Dola bilioni 2.9 unadhihirisha namna ushirikiano chini ya Mkataba wa Biashara Huria Afrika (AfCFTA) na taasisi za kifedha za kikanda unavyoweza kugeuza ndoto kubwa kuwa halisi.
Profesa Benedict Oramah, Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya Uagizaji na Uuzaji Nje ya Afrika (Afreximbank), amewaeleza wajumbe kwamba wakati Tanzania ilipotangaza mpango huo wenye lengo la kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 za umeme, kudhibiti mafuriko na kusaidia wakulima, wadau waliupokea kwa mashaka. “Taasisi za fedha za kimataifa, makampuni ya bima na wakandarasi walikataa kushiriki katika mradi huo,” amesema Oramah.
Hali ilibadilika mwaka 2018 wakati wa maonesho ya kwanza ya IATF yaliyofanyika Cairo, Misri, ambapo Tanzania ilisaini mkataba wa ujenzi na makampuni ya Misri, Arab Contractors na El-Sewedy Electric.
Bwawa lilikamilika mapema mwaka huu baada ya kuunganishwa kwa mashine ya kufua umeme ‘turbine’ ya mwisho mwezi Aprili, na sasa linauwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Katibu Mkuu wa AfCFTA, Wamkele Keabetswe Mene, aliutaja mradi huo kama kielelezo cha “mabadiliko makubwa, mafanikio makubwa zaidi chini ya mkataba wa biashara huria.”
SOMA ZAIDI
Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, amesema mradi huo unaonyesha umuhimu wa kuunganisha bara. “Tunapokutana hapa leo siyo tu kwa ajili ya jukwaa la kiuchumi, bali kusukuma ajenda ya kuhakikisha bara linaunganishwa,” amesema. Aliunga mkono wasiwasi wa Mene kuhusu changamoto za miunganisho barani Afrika, akibainisha kuwa baadhi ya washiriki walilazimika kupitia Ulaya au Asia kufika Algiers.
Takwimu rasmi zinaonyesha biashara ya ndani ya Afrika inabaki chini, ikiwa ni wastani wa asilimia 15 pekee ya biashara yote ya bara. Uwekezaji wa moja kwa moja wa ndani ya Afrika ni karibu asilimia 6, huku ushawishi wa Afrika katika maamuzi ya Shirika la Biashara Duniani ukiwa chini ya asilimia 3.
Rais Tebboune alilaumu changamoto za kimuundo, zikiwemo pengo la miundombinu ambalo alisema linaigharimu Afrika angalau asilimia 2 ya Pato la Taifa kila mwaka. “Afrika bado imetengwa katika biashara na taasisi za kifedha za kimataifa,” alisema. “Tunahitaji kutumia uwezo huu kubadilisha uchumi wetu na kutengeneza ajira kwa mamilioni ya vijana wetu.”
Maonesho ya IATF2025 yameandaliwa kwa pamoja na Afreximbank, Tume ya Umoja wa Afrika na Sekretarieti ya AfCFTA. Waandaaji wanasema zaidi ya washiriki 35,000 na waoneshaji 2,000 kutoka nchi 140 wanatarajiwa kushiriki jijini Algiers, huku mikataba ya biashara na uwekezaji yenye thamani ya takribani Dola bilioni 44 ikitarajiwa kusainiwa.