CBE yashukuru mwitikio harambee mabweni ya wasichana

CBE yashukuru mwitikio harambee mabweni ya wasichana

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimesema mwitikio wa wadau kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana katika kampasi yake mkoani Mbeya imekuwa ya kutia moyo.

Hayo yalisemwa Jumatano chuoni hapo Dar es Salaam na Profesa Emmanuel Mjema, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kilele cha harambee hiyo inayotarajiwa kufanyika Jumamosi hii jijini Mbeya.

“Tunashukuru mwitikio umekuwa mzuri na mkubwa, watu wamejitoa kuendelea kuchangia na wengine wamethibitisha watakuja Mbeya kushiriki harambee, hivyo tunawashukuru na kuwataka wengine waendelee kuchangia,” alisema.

Advertisement

Vilevile, alisema CBE imekamilisha ujenzi wa kampasi yake mkoani Mbeya yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,000 na mpaka sasa imeshachukua wanafunzi 1,000 tayari kwa kuanza masomo.

Alisema majengo ya chuo hicho yanatarajiwa kuzinduliwa Oktoba 8 mwaka huu jijini Mbeya na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Alisema majengo yaliyokamilika ni ya utawala, kumbi za mihadhara, maktaba na ofisi za wafanyakazi na yamegharimu Sh bilioni 1.46 ambazo zimetokana na mapato ya ndani.

Alisema wanafunzi wa kike wanaishi kwenye mazingira magumu kwani wengi wao wanaanza chuo wakiwa na umri mdogo na ndiyo sababu wametoa kipaumbele kwao kujengewa bweni.

Profesa Mjema alisema kilele cha harambee ya kujenga mabweni ya wasichana itafanyika Jumamosi hii jijini Mbeya na mgeni rasmi atakuwa Spika wa Bunge ambaye ndiye mlezi wake, Dk Tulia Ackson.

Aliwashukuru wadau ambao tayari wamechangia na wengine kutoa ahadi zao na kuwataka wanaoweza kuchangia kutumia akaunti ya NMB namba 20601100030 au MPESA 977992.

CBE ina kampasi tatu za Mbeya, Mwanza na Dodoma na ya nne ujenzi wake unatarajiwa kuanza Novemba baada ya chuo hicho kukabidhiwa eneo na Serikali ya Zanzibar.

 

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *