CBE yatafuta Sh bilioni 1.2 bweni la wasichana

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE) kimeandaa harambee ya kukusanya Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wasichana kampasi ya Mbeya.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emmanuel Mjema, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu harambee hiyo yenye kauli mbiu “Changia zaidi ya harusi, uwe sehemu ya kuleta tabasamu kwa watoto wa kike’.

Alisema wameamua kuanza na ujenzi wa hosteli za wasichana kutokana na changamoto wanazopata wanapokuwa nje ya kampasi kulinganisha na wavulana.

Alisema kilele cha harambee hiyo inayosimamiwa na mlezi wa Kampasi hiyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson itakuwa Septemba 24 jijini Mbeya.

Profesa Mjema alisema wanafunzi wengi wa ngazi ya diploma na cheti bado ni wadogo hivyo wanahitaji mazingira mazuri ya kusomea ndani ya kampasi hiyo.

“Siyo kwamba tunawatenga wanafunzi wa kiume bali tunazingatia hali halisi na mazingira yalivyo ndiyo maana tumeamua kuanza na hosteli za  wasichana na baadaye tutajenga za kiume,” alisema.

Aidha, alisema chuo kimefanya jitihada za kuwafikia wadau mbalimbali zikiwemo taasisi na mashirika ya serikali, yasiyo ya serikali na sekta binafsi kuomba michango.

Aliwashukuru wadau mbalimbali ambao wameshachangia ujenzi huo na wengine wametoa ahadi zao kufanikisha ujenzi huo.

Aliwataja baadhi yao kuwa ni Benki ya NMB, WMA, BRELA, TBS, NHC, Chuo Kikuu cha St John, wajumbe wa bodi ya uongozi CBE, wahitimu wa CBE, wanafunzi wa sasa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ambaye ametoa Sh milioni tano.

Aliwaomba wasamaria wema kuchangia ujenzi huo kupitia akaunti ya NMB 20601100030, TigoPesa 0710 999237 na kupitia akaunti ya MPESA ambayo ni 0742 135979.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button