CBT yafafanua taarifa pembejeo zilizoisha muda

MTWARA: BODI ya Korosho Tanzania (CBT) imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyotolewa na moja ya chombo cha habari nchini kuhusu wakulima wa korosho kupatiwa pembejeo za korosho zilizokwisha muda wake kwa msimu wa kilimo mwaka 2024/2025.

Akizungumza mkoani Mtwara juu ya ufafanuzi wa taarifa hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Francis Alfred amesema kwa niaba ya serikali waliratibu usambazaji wa viuatilifu vya ruzuku vya zao hilo mbavyo ni salfa ya unga tani 41,263 na viuatilifu vya maji lita 2,689,581 kwa wakulima hao.

Lengo ni kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu wa zao hilo nchini na kati ya hivyo lita 4,500  za (Sky plus 550EC) vyenye viambata amilifu vilisambazwa katika mkoa wa Katavi kwa ajili ya kutumika mwaka 2024/2025.

Hata hivyo, kupitia zoezi la tathmini ya usambazaji wa pembejeo kwa msimu huo wa mwaka 2024/2025, CBT iliweza kubaini kiasi cha viuatilifu hivyo vya sky plus ambavyo vimeisha muda wake wa matumizi mwezi Machi, 2025 kubaki kinyume na matarajio kwamba wakulima wangevitumia katika msimu huo wa mwaka 2024/2025.

 

Kufuatia hali hiyo wakulima walielekezwa kutovitumia wakati huku bodi ikiendelea na utaratibu wa kuvikusanya viuatilifu hivyo ili kutoa fursa ya kusambazwa kwa viuatilifu vingine vipya ambavyo viko ndani ya muda wa matumizi kwa ajili ya msimu wa mwaka 2025/2026’’amesema Francis

Aidha zoezi hilo la ukusanyaji wa viuatilifu hivyo tayari lilishaanza na linatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi Aprili mwaka huu ili kutoa nafasi ya kusambaza viuatilifu vingine vya ruzuku kwa ajili ya misimu huu wa mwaka 2025/2026.

Ametoa rai kwa  wakulima hao nchini kuhakikisha wanapopata mgawo wa viuatilifu  wavitumie ndani ya msimu husika ili kuepuka kubaki navyo na hatimaye kufikia ukomo wa muda wake wa matumizi kwani serikali kila mwaka hupanga bajeti ya kununua viuatilifu vipya kwa ajili kuwasambazia wakulima ili wavitumie ndani ya msimu husika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button