CCM: Chama tawala kikishinda uchaguzi pia ni demokrasia

DAR ES SALAAM:CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka watu hususani vyama vya kuachana na kasumba ya kusema kwamba chama tawala kikishinda uchaguzi si demokrasia lakini kikishinda ndiyo demokrasia.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla amesema hayo leo Aprili 30,2025 wakati akizungumza na wananchi katika Uwanja wa Madenge Wilaya ya Temeke Dar es salaam, akihitimisha ziara yake ya siku tatu katika mkoa huo.
Makalla ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es salaam amekuwa na ziara fupi iliyofanyika katika Wilaya tatu ya Ubungo, Kinondoni na Temeke akifanya mikutano ya hadhara kuzungumza na wananchi wa wilaya.
Akizungumza na wananchi wa Temeke Makalla amesema katika uchaguzi Mkuu Tume Huru ya Uchaguzi itatenda haki na CCM wanataka kweli watende haki na kuwataka watu kuachana na desturi wanayojiwekea kuwa chama tawala kikishinda uchaguzi si demokrasia.
“Kwa Tume hii ilivyohuru itatenda haki na sisi tunataka itende haki, maana kuna tabia imejengwa kwamba chama tawala kinaposhindwa ndiyo demokrasia ya kweli wakubali pia chama tawala kinaposhinda ni demokrasia ya kweli,” amesema Makalla.

Pia Makalla amesema CCM haijiweki madarakani yenyewe bali inawekwa madarakani na wannachi kupitia sanduku la wapiga kura na hadi wanaaminika ni kutokana na rekodi yao ya utendaji wa kazi mzuri na kuwapelekea wananchi maendeleo wanayoyahitaji.
Makalla amesema hitaji kubwa la wananchi ni maendeleo na ndiyo sababu inayowafanya wananchi wanaendelea kuiamini CCM katika chaguzi nyingi zinazofanyika.
Aidha, Makalla amesema kuwa katika serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeongoza kwa kutoa fedha nyingi ili kukamilisha miradi ya maendeleo katika maeneo na sekta mbalimbali ukulinganisha na awamu nyingine.

Makalla amesema ili kuendelea kuwa na ushawishi kwa wananchi kuelekea uchaguzi CCM itawapelekea wananchi ilani nzuri inayoendana na utatuzi wa changamoto zao na kufanya kampeni za kistaarabu kwa kuzingatia 4R za Rais Samia.



