CCM Geita yaonya fitina, visasi Uchaguzi Mkuu

GEITA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita kimewataka wanachama wake kuacha kupandikiza chuki na visasi kwa wagombea waliopitishwa kuwakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka 2025.
Aidha uongozi wa CCM mkoa na wilaya ya Geita umeahidi kuwachukulia hatua kali wale wote ambao watabainika kuendekeza makundi ingali mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama tayari ulishakamilika.
Viongozi hao wa CCM walitoa kalipio hilo Agosti 25, 2025 mara baada ya wagombea ubunge majimbo ya wilaya ya Geita kupitia CCM kukamilisha zoezi la kuchukua fomu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Wagombe hao ni Mhandisi Chacha Wambura kutoka jimbo la Geita mjini, Mhandisi Kija Ntemi wa jimbo la Katoro, Joseph Msukuma wa jimbo la Geita na Dkt Jaffary Rajab mgombea ubunge jimbo la Busanda.
Akitoa angalizo hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicolous Kasendamila amesema hawapo tayari kuruhusu fitina kwa wanachama wake na atakayebainika atawajibishwa mara moja bila kujali nafasi yake.

Kasendamila amesema mara baada ya uchaguzi wa ndani umezingatia weledi ili kupata wagombea wenye uwezo na ushindani wa kukiwakilisha chama hivo watia nia wote waliokuwepo wanapaswa kuungana.
“Anayeendekeza makundi ni sawa na mchawi ndani ya familia, na hatuwezi kuishi na mchawi ndani ya familia ya CC, nasi tutamungoa kabla hata hajatuharibia”, amesema Kasendamila.

Mgombea ubunge (CCM) Jimbo la Geita Mjini, Mhandisi Chacha Wambura amesema kuelekea hatua ya uzinduzi wa kampeni anaenda na ajenda ya Kazi na Matokeo ili kufanikisha utekelezaji wa ilani ya CCM.
Amesema alishawasiliana na wapinzania wake wakati wa mchakato wa kura za maoni na wamemuhakikishia kumuunga mkono kufanikisha utekelezaji wa ajenda hiyo iwapo atashinda ubunge.
Naye Mgombea Ubunge (CCM) Jimbo la Katoro, Mhandisi Kija Ntemi amesema Imani aliyopewa kugombea jimbo jipya la Katoro atahakikisha anailipa kwa kusikiliza na kuunganisha watu kufanikisha maendeleo.
Aidha Mgombea ubunge (CCM) jimbo la Busanda, Dkt Jaffary Rajab amesema kugombea ni hatua ya awali inayohitaji mshikamano kuekelea kuifanya Busanda kufikia matamanio ya wengi ya kukua zaidi kiuchumi.
Kwa upande wake Mgombea ubunge (CCM) jimbo la Geita, Joseph Msukuma amesema kwa uzoefu wa kisiasa alionao haoni sababu ya kumchukia mpinzani wake bali yupo tayari kuwashika mkono kwa kila hatua.


