“CCM ina mengi ya kujivunia miaka 48”

DAR ES SALAAM: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina mengi ya kujivunia katika kuadhimisha miaka 48 yapo ya chama hicho, kwani kiimeendelea kuleta mapinduzi na mageuzi makubwa kiuchumi na kijamii kwa kuleta maendeleo na mabadiliko katika sekta mbalimbali.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Ueneza na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla ameeleza hayo leo Februari 2,2025 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es salaam kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 48 ya CCM yanayotarajiwa kufanyika Februari 5, mwaka huu.
Makalla amesema kuwa wakati chama hicho kikiadhimisha miaka yake 48 tangu kuanzishwa kwake kinakwenda sambamba na mambo ambayo yameweza kufanyika tangu kuzaliwa kwake ikiwemo mambo makubwa yaliyofanyika ili kutatua changamoto mbalimbali.
Amesema pia wakiadhimisha miaka hiyo wanajivunia amani na utulivu iliyoendelea kuwepo nchini chini ya amiri jeshi mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri wa Mauungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
“Tukiwa tunaadhimisha miaka 48 ya CCM tumeona uboreshaji katika sekta ya afya, vituo vya afya vinajengwa leo katika Wilaya ya Kinondoni ndani ya jimbo la Kawe lina hospitali hadi mabwe pande,” amesema Makalla.
Ameongeza kuwa katika miaka hiyo CCM imejidhihirisha kuwa ni imara kuliko wakati wowote, kwani ni chama ambacho kina wanachama wengi Tanzania na Afrika kote na kinashika nafasi ya saba kwa wingi wa wanachama duniani kwani kina wanachama zaidi ya milioni 12.



