CCM Iringa yajizatiti ushindi maeneo yasiyo na upinzani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimehitimisha kampeni zake kwa kishindo katika mtaa wa Wambi, Mafinga mjini, kikiwataka wanachama wake kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura ili kufanikisha ushindi wa kishindo, hata katika maeneo yasiyo na wagombea wa upinzani.

Akihutubia umati wa wanachama wa CCM, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, alielezea jinsi mkoa wa Iringa ulivyo ngome ya CCM kwa miaka mingi, huku asilimia kubwa ya vijiji, mitaa, na vitongoji vikiwa chini ya chama hicho.

“Mkoa wa Iringa ni ngome ya CCM na ni mkoa ambao kwa miaka mingi umekuwa ukitoa kura nyingi kwa CCM na wagombea wake, tunaoujua mkoa wa Iringa hata miti ni CCM. Kwahiyo katika uchaguzi huu tunakwenda kukamilisha ratiba tukiwa na uhakika wa kuzoa viti vingi na tutapiga kura za kishindo hata katika maeneo yasio na wapinzani,” alisema.

Advertisement

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa Daudi Yasini alisema; “Tuna vijiji 360 mkoani Iringa, ambapo 294 sawa na asilimia 82 ya vijiji vyote, CCM haikupingwa. Katika mitaa 222, CCM haijapigwa katika mitaa 174 ambayo ni sawa na asilimia 78. Vitongoji 1,641 kati ya 1,840, sawa na asilimia 89, pia CCM haina mpinzani.”

Katika maelezo yake Yasin naye alisisitiza umuhimu wa wanachama wote wa CCM kupiga kura kwa wingi, hata katika maeneo ambayo chama hakina upinzani.

“Hii itakuwa njia nzuri ya kuthibitisha kuwa CCM inajivunia siasa za maendeleo na haina mpinzani wa maana, sio tu katika uchaguzi huu bali pia kwa uchaguzi mkuu wa mwakani,” aliongeza.

Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Zuberi Ali Maulid, aliwataka wanachama wa CCM kuonyesha nguvu zao hata katika maeneo yasiyo na wagombea wa upinzani.

“Tukajitokeze kwa wingi kupiga kura. Hii ni nafasi ya kuwathibitishia wapinzani wetu kwamba kila kona ya nchi, hata maeneo ambayo hawana wagombea, CCM ina nguvu kubwa na inaungwa mkono,” alisema Zuberi.

Alisema CCM inategemea ushindi mkubwa kesho kutokana na mtaji wa utekelezaji wa Ilani ya chama katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa, huku akitaja imani kubwa ya wananchi kwa serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kama nguzo ya ushindi wake.

Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi, aliwasihi wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kazi anayofanya Rais Samia imegusa maisha ya kila Mtanzania, hususan wananchi wa kawaida. Tunahitaji kuhakikisha kura za ‘hapana’ zinazopangwa na wapinzani hazifui dafu,” alisema

Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chadema kanda ya Nyasa Leons Marto, alisema CCM imeendelea kuwajibika kwa wananchi kupitia utekelezaji wa Ilani yake, tofauti na vyama vya upinzani ambavyo alidai vimefilisika kwa hoja.

“Huwezi kuwa na chama ambacho mwenyekiti anaongea lake na makamu wake anaongea lingine. Watanzania wamewaelewa Chadema na sasa wameamua kurudi nyuma,” alisema.

Marto pia alimtaja Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, Willy Mungai, akidai hana shukrani kwa serikali ya CCM, ambayo ilihusika kwa njia moja au nyingine kulea familia yake.

“Anasimamia chama akiwa mbali, huko Kawe, Dar es Salaam, badala ya kuwa karibu na wananchi wa Iringa,” alisema kwa kejeli.