CCM Iringa yakana kauli tata ya mwenyekiti halmashauri Iringa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimejitenga na kuyakana matamshi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa, aliyodai kuwa madiwani na wabunge waliopo madarakani lazima majina yao yatarudishwa kuwa miongoni mwa wagombea.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika hivi karibuni mjini Iringa, Mhapa amenukuliwa akisema madiwani na wabunge hao ni lazima watakuwa sehemu ya wana CCM watatu watakaorudishwa katika kura za maoni za chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura.
Akizungumza na wanahabari mjini Iringa leo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin, alisema chama kimesikitishwa na kauli hiyo na kusisitiza kuwa huo sio msimamo wa CCM.
“Tunapenda kuweka wazi kwamba kauli hiyo si msimamo wa Chama Cha Mapinduzi bali ni mawazo yake binafsi. CCM haijatoa mwongozo wa aina hiyo na haukubaliki,” alisema Yasin.
Amesisitiza kuwa chama kinafuata katiba, kanuni na miongozo yake katika mchakato wa uteuzi wa wagombea, na hakuna anayependelewa moja kwa moja.
“Muda utakapofika wagombea wote watakuwa sawa na watafuata utaratibu rasmi wa chama, ambapo sifa na uwezo wao vitajadiliwa kupitia vikao husika. Hakuna anayehakikishiwa kupitishwa moja kwa moja,” aliongeza.
Kutokana na hilo alisema, Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa imewataka viongozi wa chama na wanachama kujiepusha na matamko yenye utata yanayoweza kusababisha taharuki miongoni mwa wanachama na jamii kwa ujumla.
“CCM imesisitiza kuwa inaendelea kuzingatia misingi ya demokrasia, huku ikihakikisha mchakato wa uteuzi wa wagombea unafanyika kwa haki na uwazi kulingana na katiba na kanuni za chama” alisema.



