CCM Iringa yazindua sherehe za kuzaliwa kwa kuwekeza kwa jamii

Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimezindua sherehe za miaka 48 ya kuzaliwa kwake kwa shamrashamra zilizopambwa na mshikamano wa kisiasa, ahadi za maendeleo na kauli nzito za uchaguzi ujao.

Uzinduzi wa sherehe hizo zitakazohitimishwa Februari 5 siku ya kuzaliwa kwa chama hicho, umefanyika katika kata ya Ng’uruhe wilayani Kilolo.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC) Taifa, Salim Asas, alitoa msaada wa Sh Milioni 10 kuchangia ujenzi wa Shule ya Sekondari Ng’uruhe, Sh Milioni mbili na misaada mbalimbali kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Pomerin, pamoja na ahadi ya kusaidia kukamilisha bweni la shule hiyo na ujenzi wa ofisi ya CCM ya kata hiyo.

Kwa mujibu wa viongozi wa chama hicho, Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa iliamua sherehe hizo zifanyike wilayani Kilolo kwa lengo la kuonesha miradi ya maendeleo na mshikamano wa wanachama katika eneo hilo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, MNEC Asas alisema CCM inaendelea kuadhimisha miaka yake ya kuzaliwa kwa kuwaletea wananchi maendeleo halisi na sio maneno matupu.

“CCM ni chama tawala, ni chama chenye serikali, na tunatumia nafasi hii kuwaeleza wananchi kile ambacho tumetekeleza kwa mujibu wa Ilani yetu,” alisema Asas.

Katika hotuba yake, Asas alifafanua kuwa chama tayari kimefunga mjadala wa mgombea wa urais kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM umeazimia kwa kauli moja kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ndiye mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Dk. John Nchimbi akichaguliwa kuwa mgombea mwenza.

Kwa upande wa Zanzibar alisema, Dk. Hussein Mwinyi amepitishwa kuwania muhula wa pili.

“Kwa upande wa urais, CCM imefunga pazia. Kama kuna mtu alikuwa na ndoto, asipoteze muda wake. Sasa tunasubiri Oktoba, ili wagombea wetu wapewe kura za ‘ndiyo’,” alisema Asas.

Alisisitiza kuwa chama kimefanya maamuzi hayo mapema kama sehemu ya kuenzi kazi kubwa ya maendeleo iliyofanywa na Rais Dk Samia.

Hata hivyo, alibainisha kuwa nafasi za ubunge na udiwani bado hazijafunguliwa kwa mchakato wa wagombea, akiwatahadharisha wale wanaojitangaza mapema kuwa wanakiuka taratibu za chama.

“Wanaotangaza nia ya kugombea ubunge na udiwani, muda haujafika. Acheni waliopo madarakani wamalize muda wao, kipenga kikilia, ndipo mjitokeze,” alisisitiza.

Alihimiza mshikamano na nidhamu ndani ya chama, akiwataka wanachama wenye nia ya kugombea kuepuka kuchafuana.

“Kama unataka ubunge au udiwani, usimchafue aliyepo madarakani. Subiri muda ufike, chama kitaamua kwa mujibu wa taratibu zake,” alisema.

Aidha, alitoa angalizo kuhusu umuhimu wa kuchuja wagombea kwa umakini zaidi kutokana na ongezeko la wapiga kura.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilolo, John Kiteve na viongozi wengine mbalimbali walitambua mchango mkubwa wa Rais Dk Samia katika maendeleo ya nchi, hususan katika sekta za maji, elimu, afya, miundombinu, kilimo, viwanda, biashara na utalii.

Ilielezwa kuwa kata ya Ng’uruhe imepata mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Sh Bilioni 1.6, pia, uwekezaji katika sekta ya chai, miti na mazao ya chakula na biashara ukisisitizwa kama sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha maisha ya wananchi.

“Sisi wana Kilolo tunatambua mchango wa Dk. Samia, na ahadi yetu ni moja—tutamlipa kwenye sanduku la kura uchaguzi utakapofika,” alisema Kiteve.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa, Mwanahabari Tumaini Msowoya, aliwataka wananchi kuthamini amani iliyopo nchini, akitoa mfano wa machafuko yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

“Kule Congo wenzetu hawana amani. Tujivunie tuliyonayo na pia tupeleke watoto wetu shule, tuache kukatisha ndoto zao za maisha kwa kuwapeleka kufanya kazi za majumbani mikoani,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Iringa, Agrey Tonga alisisitiza kuwa wanapoazimisha 48 ya CCM, mchango wa MNEC Salim Asas hauwezi kupuuzwa.

“Huwezi kuzungumzia maendeleo ya CCM Mkoa wa Iringa bila kumtaja Asas ambaye hivi sasa yupo katika jitihada za kuhakikisha kila kata inakuwa na ofisi ya chama. Amejitokeza kwa vitendo, na sisi tunapaswa kuiga mfano wake,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button