CCM Kibiti yaridhishwa utekelezaji Ilani
KAMATI ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Juma Ndaruke imekagua miradi ya maendeleo wilayani Kibiti mkoani Pwani na kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.
Sambamba na hilo kamati imeipongeza serikali kwa kupeleka fedha za miradi wilayani humo hali ambayo inazidi kuchochea ukuaji wa Wilaya ya Kibiti.
Miradi ya maendeleo iliyokaguliwa ni pamoja na shule za msingi za Itonga na Jaribu ambazo kila moja ina madarasa 9 pamoja na majengo ya utawala na yametengewa bajeti ya Sh milioni 306 kwa kila shule.
Mradi mwingine ni ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kibiti ambayo ujenzi wake umegawanyika kwenye maeneo manne ambayo ni jengo la upasuaji ambalo limetengewa bajeti ya Sh milioni 237, wodi ya wanawake kwa Sh milioni 235, wodi ya wanaume Sh milioni 235 na jengo la kuhifadhia maiti kwa bajeti ya Sh milioni 93
Mradi mwingine ambayo kamati hiyo ya siasa ilitembelea na kukagua ni kituo cha afya cha Nyamatanga ambacho kinajengwa kwa gharama ya Sh milioni 500 pamoja na daraja la Mbwera lenye Sh milioni 999.
Akizungumza kwenye kikao cha ndani cha kufanyia tathimini ya hali ya ujenzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibiti ambaye pia ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya, Juma Ndaruke alisema kuwa chama kimeridhika na utekelezaji wa ilani na kuwapongeza wote wanaosimamia ujenzi wa miradi hiyo.
“Nachukua fursa hii kumpongeza Rais na Mwenyekiti wa Taifa wa chama chetu mama Samia Suluhu kwa kutenga bajeti ya utekelezaji wa miradi hii ambayo hivi punde tumemaliza kukagua. Miradi hii italeta uchochezi wa maendeleo kwenye wilaya yetu ya Kibiti. Kwa niaba ya chama ngazi ya wilaya tunampongeza sana na sisi tunaahidi kuendelea kusimamia miradi hii kwa niaba ya wananchi wote wa wilaya ya Kibiti’, Ndaruke alisema.
Nawapongeza sana uongozi wa wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji kwa kuweza kusimamia ujenzi wa miradi hii.
- Hata hivyo, kwa niaba ya chama nawaomba watumishi wote wa serikali ambao wanasimamia miradi hii kuhakikisha ya kwamba inakamilika kwa wakati na na pesa zilizokususudiwa, Ndaruke aliongeza.” aliongeza