CCM Kigoma yashukuru ushindi serikali za mitaa

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Kigoma kimewashukuru wananchi mkoani humo kwa kukipa chama hicho ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomaliza hivi karibuni.

Mwenyekiti wa chama hicho mkoa Kigoma, Jamal Tamim akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Kibondo amesema kuwa ushindi huo wa asilimia 96 unaipa imani CCM kuwa kazi kubwa ya Serikali ya Rais Samia ya kupeleka maendeleo kwa wananchi inakubalika.

Tamim amesema kuwa CCM itaendelea kuisimamia serikali kuhakikisha maendeleo zaidi yanafanyika mkoani Kigoma huku akieleza kuwa mpango wa serikali kukopa fedha nje kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kunaonesha serikali kukubalika kwa wafadhili na wahisani.

Advertisement

Sambamba na hilo mwenyekiti huyo amesema wana CCM ambao hawakupata nafasi ya kupitishwa kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa bado nafasi zipo nyingi ambapo amewataka wote wenye nia ya kugombea kujitokeza kuchukua fomu muda utakapowadia.