Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa kimeanza rasmi kampeni zake za kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kishindo, baada ya kumpokea aliyekuwa Katibu wa Uenezi wa Chadema Kanda ya Nyasa, Leons Marto, ambaye sasa amehamia CCM.
Katika tukio hilo lililovuta hisia za wengi, mgeni rasmi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mohammed Abood, alieleza kuwa Marto ni mwanzo wa wimbi kubwa la wanachama kutoka vyama vya upinzani kurudi CCM, akisema hata Tundu Lissu yupo njiani kujiunga nao.
“Chama kimefilisika, hakina ajenda. Yule mwamba Mbowe amechoka, asije akaanguka kwa presha. Huku CCM imethibitika kuwa chombo madhubuti cha kuongoza maendeleo ya taifa,” alisema Marto.
Alisema kuwa Chadema kimepoteza mwelekeo na hakina tena misingi iliyokuwa inakisimamia.
Alieleza kuwa ameamua kurudi CCM kwa sababu ni chama pekee chenye mfumo thabiti wa kutatua changamoto za wananchi.
“Nilichokiamini na kukipenda ndani ya Chadema hakipo tena. Chama kimebaki na utapeli na siasa za maneno. Niko tayari kuingia kazini leo hii kuhakikisha CCM inashinda kila eneo,” alisema Marto huku akihimiza maridhiano na mshikamano wa Watanzania.
Abood alimwelekeza Marto kuanza kampeni mara moja kwa kushirikiana na viongozi wengine wa CCM, akisisitiza kuwa Marto ana nguvu ya kufanya kazi mtaani na kuwahamasisha wengine walio kwenye vyama vya upinzani kurejea CCM.
Abood alitumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi wa Iringa kuendelea kuiamini CCM, akisema Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameleta maendeleo makubwa nchini, yakiwemo kupambana na umasikini, maradhi, na ujinga.
“Mama Samia ameonesha mfano wa uongozi bora. Angalia Iringa ya leo na ya jana, tofauti ni kubwa. Tuko hapa leo kusherehekea mafanikio haya na kuhakikisha tunalinda amani na maendeleo yanayoletwa na CCM,” alisema Abood.
Alieleza kuwa CCM inaendelea kutekeleza ilani yake kwa mafanikio makubwa, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, maendeleo ya kilimo, na kukuza sekta ya utalii mkoani Iringa.
Lissu na wengine watajwa
Katika hotuba yake, Abood alisisitiza kuwa Lissu, pamoja na wanachama wengine maarufu wa upinzani, wanasubiriwa CCM kwa sababu wanatambua kuwa hakuna mustakabali wa kisiasa nje ya chama hicho.
“Sisi tunataka chama cha kushindana nacho, lakini kule upinzani hakuna tena watu wa maana. Kwa hiyo, tunawakaribisha wote wanaotaka kushirikiana nasi kujenga Tanzania mpya,” alisema Abood.
Alisena CCM imeahidi kujenga mazingira bora ya kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo kuhakikisha barabara zote, kama ile ya Ruaha, zinajengwa kwa viwango vya juu. Pia, mkoa huo utaimarishwa kama kituo kikubwa cha utalii, kilimo, na huduma za afya.
“Tutashirikiana na wananchi kusikiliza kero zao na kuzitatua. Msingi wa maendeleo ni ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na viongozi wa CCM,” alisisitiza Abood.
Katika mkutano huo viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu wamewataka wanachama wao kusimama imara kuhakikisha wagombea wao wanapita katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kishindo.
Viongozi hao wamesema kwa pamoja watashirikiana na wananchama wao katika kila mtaa okaWananchi kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba na kitanda kwa kitanda ili kuhakikisha ushindi mkubwa wa CCM.