CCM yagusia zao la pamba

MASWA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kuisimamia na kusisitiza serikali kuhakikisha bei ya pamba inamnufaisha mkulima.

Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi ameeleza hayo leo Maci 7,2026 alipotembelea mradi wa shamba la pamba lililopo katika  Kijiji cha Mwantumbe Kata Shishiyu wilayani Maswa mkoani Simiyu.

Kihongosi amesema Mkoa wa Simiyu unatambulika kwamba pamba ni dhahabu nyeupe, pamba ni uchumi, pamba ni fedha, hivyo wataibeba ajenda ya wakulima wa pamba na mazao mengine yakiwemo tumbaku na waweze kuona tija katika kilimo, kwani kilimo ni uti wa mgongo wa taifa.

“Na sisi tutazidi kuisisitiza serikali kama chama kwa kuhakikisha bei ya pamba inamnufaisha mkulima, hili tutalibeba kama ajenda ili wakulima wa pamba na mazao mengine yakiwemo tumbaku na kadhalika waweze kuona tija katika kilimo,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa serikali imejaribu teknolojia nzuri, imewashughulikia na kuwajali wakulima kwa kilimo cha kisasa na kitaalamu, lengo ni kuendelea kuachana na kilimo cha zamani.

Amesema kazi ya chama ni kusimamia utekelezaji wa Ilani, kwa sababu haya yanayoonekana na kufanyika yapo ndani ya Ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2025/30 kwamba watakwenda kuboresha kilimo na kuboresha miundombinu yake. 

“Sasa miundombinu ndiyo inaonekana, huduma serikali inafanya na pia viongozi wanaendelea kusimamia, sisi kama chama tumefika hapa tumefarijika kuona utekelezaji wa Ilani katika Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Maswa unaenda vizuri,” amesema Kihongosi.

Awali Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Kiseto amesema serikali imekuwa ikisaidia wakulima wa pamba wilayani huko kwa kuwakodishia matrekta na ndege nyuki kwa ajili ya kumagilia dawa ili kuzuia mazao hayo yasiliwe na wadudu.

Ilielezwa teknolojia hiyo imesaidia kuongeza uzalishaji kutoka kuvuna kilo 200 za pamba hadi 1000 kwa ekari moja hatua ambayo ni mafanikio makubwa, pia serikali imeombwa iendele kuwangalia kwa kuwasaidia hata mikopo ya matrekta wakulima wa pamba.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button