CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuw hakitatumia nguvu kubwa kuwanadi wagombea wake wa nafasi ya uenyekiti wa vitongo na vijiji kwani kazi kubwa ya kupeleka maendeleo kwa wananchi kupitia utekelezaji wa ilani inatosha kuipa ushindi CCM.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Christopher Gachuma amesema hayo Novemba 20 wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakati akizundua kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa akimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Gachuma amesema kuwa miradi iliyotokelezwa na serikali inayotokana na ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 imegusa maisha ya wananchi wa kawaida ikiwemo miradi ya maji,afya, elimu, barabara, miradi ya umeme lakini pia uwezeshaji wananchi katika masuala ya kiuchumi na kilimo.
Awali kabla hajamkaribisha mgeni rasmi kuzindua kampeni hizo Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kigoma, Jamal Tamim alisema kuwa mkoa umeweka mkakati kuhakikisha wanashinda vijiji 306 vya mkoa Kigoma ambapo katika vijiji 34 na vitongoji 700 vyama vya upinzani havina wagombea.
Akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa kampeni hizo Mkuu wa Mkoa, Thobias Andengenye alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wagombea na vyama vyao wanapewa nafasi sawa katika kuendesha kampeni zao kwa amani kulingana na sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi zilizowekwa.
Andengenye alisema kuwa anakemea kauli yeyote ambayo itazuia wananchi, wagombea au viongozi wa vyama kuhudhuria mikutano ya kampeni na kwmba wanataka sera za vyama ndiyo ziongoze kampeni hizo badala ya vitisho na kuzuia taratibu za kufanya kampeni hadi kupiga kura na ikitokea vyovyote wapewe taarifa ili wachukue hatua.