CCM yavipa somo vyama vyenye ruzuku

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimetoa wito kwa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku kutumia sehemu ya fedha hizo kuchangia shughuli za maendeleo katika jamii.

Wito huo umetolewa leo na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa Joseph Lyata alipozungumza na waandishi wa habari mjini Iringa.

“Kama ilivyo katika vitabu vya dini, inaagizwa kutoa fungu la kumi kama sadaka na kusaidia shughuli za kijamii; navisihi vyama vya siasa vinavyopata ruzuku navyo vichangie fungu la kumi katika shughuli za maendeleo,”amesema.
Kwa upande wa CCM amesema wanatekekeza wajibu huo huku akitoa mifano mbalimbali ukiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo la usafi katika hospitali ya wilaya ya Iringa pamoja na vifaa vyake muhimu ikiwemo mashine za kufulia, kuchoma taka na kuiunganisha na huduma ya Televisheni ili wateja wake waendelee kujionea yanayoendelea nchini na duniani wakati wakipata huduma.

Advertisement

“Yapo mengine mengi ambayo tumefanya kuchangia maendeleo ya watanzania wenzetu, huu ni mfano kwa vyama vingine vya siasa kushiriki shughuli za mandeleo badala ya kuwa walalamikaji tu,” alisema.

Katika hatua nyingine Lyata amewataka viongozi wote wa CCM mkoa wa Iringa waliochaguliwa na wananchi katika nafasi za uwakilishi kufanya mikutano ya hadhara kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

“Kazi hii isiachwe kwa Mwenyekiti wetu Dk Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa chama. Tunataka ifanywe na viongozi wote wakiwemo wawakilishi wa wananchi katika vikao vya maamuzi,” alisema.

Amesema kuwa wenyeviti wa vijiji na mitaa, madiwani na wabunge wanapaswa kuwapa wananchi mrejesho wa shughuli wanazofanya na kujibu hoja za upinzani katika maeneo yao hasa hoja za upotoshaji kuhusu shughuli za maendeleo zinazofanywa na serikaliya awamu ya sita.

2 comments

Comments are closed.