DAR ES SALAAM:MKURUGENZI wa Programu za Maendeleo na Utetezi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Azgard Stephen alipendekeza kuimarishwa kwa nafasi ya uhusiano wa kidiplomasia kiwe kama kichocheo cha maendeleo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Azgard ametoa kauli hiyo leo Januari 13, 2025 wakati wa Mkutano wa Kamati ya Dini Mbalimbali chini Tanzania, uliofanyika Dar Es salaam kuhakiki rasimu ya kwanza ya Dira 2050, ikiwa ni Kundi la Mwisho kufikiwa na Tume ya Mipango kwaajili ya Mapitio ya rasimu hiyo.
“Sisi CCT tuliangalia suala la sayansi na teknolojia kwa kuzingatia jinsi dunia ilivyobadilika na mapinduzi yanayotokea, hivyo tunapendekeza diplomasia iwe sehemu ya vichocheo vya maendeleo ili kuwezesha Tanzania kujihusisha vyema katika biashara za kimataifa na kujitengenezea nafasi bora kikanda na kimataifa,” alisema Azgard.
Azgard ameelezea kuwa mapinduzi ya kidijiti ni mojawapo ya vichocheo muhimu vya maendeleo vilivyotajwa katika rasimu ya Dira hiyo, akibainisha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika teknolojia na sayansi ili kufanikisha malengo ya Taifa.
Msemaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Camilius Kasala amesisitiza umuhimu wa kuzingatia familia na vijana kama nguzo kuu za maendeleo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kufanikisha kuwa na maendeleo endelevu.
Dk Kasala amesema ni muhimu dira kuweka mikakati ya mazingira bora kwa familia na vijana kushiriki katika sekta za uvuvi, kilimo, ufugaji, na ufundi kwa kuzingatia hali ya hewa na jiografia ya maeneo yao. Pia ametoa wito wa kuwepo kwa elimu ya watu wazima itakayowawezesha familia kushughulikia changamoto za killa siku za kijamii.
Pia wamependekeza kuwa kuelekea 2050 ni muhimu kama Taifa kuwa na huduma za kifedha jumuishi na ambazo pia zitazingatia sheria za kiislamu ili kutengeneza usawa bila ya ubaguzi wa kidini.
Wameshauri kuwa ni muhimu serikali kuhakikisha inaweka mkazo kudhibiti michezo ya kamari kutokana na namna inavyoua nguvu kazi ya jamii na kuwatia Vijana wengi kwenye umaskini wa Kipato.
Pia wamesisitiza juu ya umuhimu wa kutilia mkazo kilimo cha mageuzi na Kilimo biashara kuanzia ngazi ya Familia ili kuhakikisha kuwa kilimo kinakuwa na tija kiuchumi na kuwa sehemu ya kuwaondoa watanzania kwenye lindi kubwa la umaskini lililopo kwenye jamii nyingi hasa jamii ya wakulima.
Katika vichocheo vya maendeleo ardhi imezungumzwa kwa uchache sana, lakini waliona dira iweke umuhimu wa kurasimisha ardhi ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi. Pia kuwe na uchumi jumuishi usioweka matabaka kati ya wenye nacho na wasionacho na kuwa na uchumi shindani kwa kulenga mbali matarajio kuelekea 2050.
Mwisho.