MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi amesema wananchi wachague viongozi wanaotokana na chama hicho ili kusimamia mikopo ya asilimia 10 inayotengwa na halmashauri.
Ntobi aliyasema hayo jana kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kimkoa katika Kata ya Masekelo iliyopo Manispaa ya Shinyanga ambapo alisisitiza zifanyike kampeni za kistaarabu na kuwataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioko madarakani watende haki katika suala la ulinzi na usalama.
Ntobi alisema vijana wengi hawana ajira wako mitaani, hivyo wanategemea kufanya biashara na viongozi watakaochaguliwa wahakikishe kundi la vijana linapata mikopo kiuhakika ili waondokane na maisha duni waliyonayo.
Isome pia:Samia arudisha mikopo ya asilimia 10
Alisema kuhusu ushuru wa taka za majumbani, maeneo ya biashara na viwandani unaotozwa na halmashauri watahakikisha maeneo ya majumbani hayatozwi kwani zitatumika fedha za ushuru wa halmashauri kufidia ushuru unaotozwa kwa kila nyumba.
“Nimesema safari hii wananchi msikubali mtu ambaye hajashinda ujumbe au nafasi ya mwenyekiti atangazwe, hivyo tunaomba usimamizi uwe wa haki, tutakubali matokeo kama tutaona ucha guzi umefanyika kwa haki,” alisema Ntobi