Chadema yajipanga kujaza nafasi za waliohama
KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokutana Mei 23 na 24, 2025 imeazimia mambo kadhaa ikiwemo kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na kuhama kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho.
Hayo yalielezwa jana mkoani Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche kwenye Kongamano la Jumuiya ya Wanafunzi wa Chadema Vyuo Vikuu (CHASO) Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema Kamati Kuu (CC) imekitaka chama kusimamia na kuhakikisha nafasi zote zilizoachwa wazi kwenye chama na mabaraza zinajazwa ndani ya siku 14 kuanzia Mei 25, 2025.
“Kuna watu wameondoka wakifikiri wao ni maarufu sana kuliko chama… wameshangiliwa sana kupitia Chadema wakafikiri wao ni maarufu lakini hawajawahi kupata hata kura za kumfaa udiwani na ubunge,” aliongeza Heche.
Aidha, alisema azimio lingine ni chama kuendelea kutoa mafunzo kwa viongozi wa kanda na mikoa ambayo haijafanya mafunzo hayo kama vile Kanda ya Pwani, Kaskazini na Kanda ya Unguja, Pemba na Nyasa.
Alisisitiza kwa kanda ambazo zimeshafanya mafunzo, viongozi wa kanda waendelee kutoa mafunzo kwa ngazi ya jimbo, kata na matawi na kwamba mafunzo yanaendelea kufanyika kila siku na yataendelea.
Aliongeza kuwa Kamati Kuu ya chama hicho imeridhia chama kianze utaratibu wa Tuzo za Uongozi mwaka 2025 ili kujenga viongozi vijana kwa ajili ya chama na taifa.
Mwenyekiti wa Chaso, Leonce Martin aliiomba serikali kuweka mazingira rafiki kwa vijana kushiriki katika siasa za nchi ili taifa lipate viongozi bora, wazalendo na wanaothamini nchi yao.
Alisema hata waasisi wa taifa walipata nafasi ya kufanya siasa mpaka wakafanikiwa kulikomboa taifa kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rashid Kawawa, Edward Moringe Sokoine na wengineo.
Baada ya kukamilisha uchaguzi mkuu wa chama na kuchaguliwa kwa Tundu Lissu kuwa Mwenyekiti wa Chadema kwa kumshinda Mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe, Chadema iligawanyika na kuwa katika pande mbili baada ya kuibuka kwa kundi la viongozi na wanachama waliojiita G55.
Kundi hilo likiongozwa na Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje wa zamani wa chama hicho, John Mrema na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu lilipinga kuzuia uchaguzi kupitia kauliumbiu ya Hakuna Mabadiliko Hakuna Uchaguzi.
Baada ya uongozi wa Chadema kulipuuza kundi hilo likiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila hatimaye liliamua kukihama chama na kwenda kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) chini ya uenyekiti wa Hashim Rungwe.
Mbali na hao, viongozi mbalimbali wa chama katika kanda pia walikihama chama hicho na kujiunga na Chaumma na wengine ACT Wazalendo.



